Museveni ajitokeza hadharani baada uvumi kuhusu afya yake

Museveni ajitokeza hadharani baada uvumi kuhusu afya yake

Na MASHIRIKA

ENTEBBE, UGANDA

RAIS wa Uganda, Yoweri Museveni Jumapili alionekana hadharani siku mbili baada ya uvumi kuenea kwamba kiongozi huyo mkongwe alilazwa hospitalini Kenya au Ujerumani akiugua maradhi yasiyojulikana.

Ripoti hizo ziliibuka siku moja baada ya Museveni, 76, kuamua kuongeza masharti makali zaidi ya kuzuia maambukizi ya virusi vya corona nchini humo.

Hii ni baada ya taifa hilo kushuhudia ongezeko la visa vya maambukizi ya ugonjwa huo hatari kutokana na msambao wa aina mpya ya virusi hivyo.

Watumiaji kadha wa mitandao ya kijamii ya twitter na Facebook walituma jumbe zilizodai kuwa Rais huyo wa Uganda alisafirishwa nje kwa matibabu baada ya afya yake kudhoofika.

Baada ya kubainika kuwa habari hizo hazikuwa za ukweli, Shirika moja la habari nchini Uganda lilishauri umma kuzipuuzilia mbali. Liliomba msamaha kwa kuweka taarifa kuhusu suala hilo kwa mtandao wake wa twitter.

Lakini Jumapili, Rais Museveni alionekana akihutubu katika Mkahawa wa Speke Resort katika kitongoji cha Munyonyo ulioko karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebbe. Alikuwa amepangiwa kufungua rasmi mkutano wa kikanda wa viongozi wa muungano wa Afya Ulimwenguni (World Health Summit).

Kiongozi huyo alionekana akiingia ndani ya ukumbi wa mkutano akiandamana na mkewe, Janet Museveni.

Mkutano huo wa viongozi umepangwa na Chuo Kikuu cha Makerere kwa ushirikiano na serikali ya Uganda. Baadhi ya masuala yanayojadiliwa katika mkutano huo yanayohusu juhudi za Afrika kutimiza Malengo ya Umoja wa Mataifa kuhusu Maendeleo Endelevu na mpango wa afya kwa wote (UHC).

Mada zinazojadiliwa ni pamoja na; Afya ya Vijana Afrika, Ukumbatiaji wa Teknolojia katika sekta ya Afya Afrika, Mbinu za Kupambana na Magonjwa ya Kuambukiza, Udhibiti wa Magonjwa yasiyo ya Kuambukiza, miongoni mwa mada zingine.

Wakati huo huo, Rais Museveni ametangaza kuwa Uganda haitahitaji misaada ya chanjo ya Covid-19 kwa sababu iko katika hatua za mwisho za kuanzisha mradi wa kuzalisha chanjo hiyo kivyake.

Kufikia sasa, Uganda imepokea dozi milioni moja za chanjo aina ya AstraZeneca kutoka kwa mpango wa kutoa msaada wa chanjo kwa mataifa masikini, COVAX, na serikali ya India.

Nchi hiyo inalenga kutoa chanjo hiyo kwa karibu raia wake 26 milioni ili kuwakinga dhidi ya maambukizi ya ugonjwa huu hatari.

Kulingana na Rais Museveni, nchini hiyo itaanza kuzalisha chanjo ya corona kwa wingi zaidi mnamo Oktoba mwaka huu.

“Hatutaki misaada ya chanjo. Kile tunahitaji ni malighali pekee. Tutanunua malighali hiyo na kuanza kujitengenezea chanjo yetu hivi karibuni,” akasema mbele ya viongozi wa ulimwengu wanaohudhuria mkutano huo. Uganda inaandaa mkutano huo kwa mara ya kwanza.

You can share this post!

Jinsi ya kuandaa mandazi ya mdalasini

Domodomo nje, mabubu ndani