Museveni akabidhiwa nakala za kesi ya Bobi Wine kutaka ushindi wake ufutiliwe mbali

Museveni akabidhiwa nakala za kesi ya Bobi Wine kutaka ushindi wake ufutiliwe mbali

DAILY MONITOR Na SAMMY WAWERU

Mawakili wa kiongozi wa chama cha NUP, Robert Kyagulanyi wamemkabidhi Rais Yoweri Museveni (NRM) nakala za kupinga ushindi wake, kufuatia kesi waliowasilisha katika mahakama ya juu zaidi Uganda mnamo Jumatatu.

Bw Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine anaitaka mahakama kufutilia mbali ushindi wa Rais Museveni, akidai shughuli ya uchaguzi mkuu nchini humo uliofanyika mnamo Januari 14, 2021, ilisheheni utapeli na wizi wa kura.

Kulingana na matokeo yaliyotangazwa rasmi Januari 28 na tume ya uchaguzi Uganda, UEC, Bw Museveni aliibuka kidedea kwa zaidi ya kura milioni sita (asilimia 58 ya kura zilizopigwa), akifuatwa na Wine ambaye alizoa kura 3.6 sawa na asilimia 35.

Katibu Mkuu wa chama cha NRM, na ambacho kinaongozwa na Rais Museveni, Bi Justine Kasule Lumumba, alipokea nakala za kesi hiyo katika afisi za mahakama ya juu zaidi zilizoko Kololo, Kampala.

Aidha, imebainika kuanzia Jumanne mawakili wa Bobi Wine wamekuwa wakijaribu kumfikia Rais Museveni binafsi wampokeze nakala hizo bila mafanikio.

Bi Lumumba hata hivyo alisema isingewezekana kumfikia Rais kwa sababu hakuwa ameamuru kampuni ya mawakili itakayomwakilisha kupokea nakala za kesi hiyo.

“Kisheria hawapaswi kumkabidhi mgombea, ikiwa hajaagiza wakili au mawakili wake. Kufikia Jumanne, hakuna yeyote aliyekuwa amepata agizo kutoka kwa mgombea,” alisema katibu huyo mkuu wa NRM.

Mawakili wa Wine wameeleza kupata afueni baada ya NRM kupokezwa nakala za kesi kupinga ushindi wa Rais Museveni.

“Hatimaye tumepata afueni, tulikuwa tumezunguka Kampala nzima tukitafuta mpokezi wa kwanza tumkabidhi nakala yeye binafsi kwa mujibu wa sheria,” wakasema.

Rais Museveni ana makataa ya hadi Ijumaa, Februari 5, 2021 kujibu madai ya Wine.

Wengine waliopokezwa nakala za kesi hiyo ni tume ya uchaguzi Uganda, UEC na mwanasheria mkuu.

Akitetea malalamishi yake, anayoshikilia zoezi la uchaguzi halikuwa la huru, haki na wazi, Bobi Bobi Wine anadai maafisa wa jeshi Uganda walikuwa wakiingia kwenye vituo vya kupigia kura na kutia karatasi za kura zilizo na alama ya kuchagua Museveni, kwenye masunduku.

Rais huyo ambaye ametawala Uganda kwa kipindi cha muda wa miaka 34 mfululizo, kuanzia 1986, umetajwa kama wa kimabavu na kidikteta kutokana na anavyohangaisha wapinzani wanaomletea ushindani katika uchaguzi.

Tangu Wine atangaze azma yake kuwania urais, amekuwa akikamatwa mara kwa mara na maafisa wa usalama Uganda na kupitia mateso.

You can share this post!

CORONA: Liverpool hawawezi kusafiri Ujerumani kwa mchuano...

Brigid Kosgei sasa kuwa balozi wa kutangaza Stanbic Bank