Kimataifa

Museveni akemewa wazee kumpigia magoti kijijini

January 9th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

KIONGOZI wa Uganda Rais Yoweri Museveni ameshutumiwa vikali baada ya video kuchipuza mtandaoni ikionyesha wazee wakimpigia magoti kabla ya kuwapa fedha.

Video hiyo inaonyesha watu wakiimba na kupiga ngoma huku wazee wakijitokeza mmoja baada ya mwingine wakipiga magoti na kisha kupokea bahasha inayoaminika kusheheni fedha.

Kulingana na Rais Museveni, wazee waliopewa fedha hizo walimsaidia kupigana msituni na kufanikiwa kutwaa uongozi wa nchi hiyo kutoka kwa mtangulizi wake, Apollo Milton Obote.

Kiongozi wa upinzani Kizza Besigye alikashfu Rais Museveni akisema kuwa alidhalilisha wazee hao.

“Ni aibu kwa wazee kupiga magoti ili kupata fedha kidogo kwenye bahasha. Ili kukomesha aibu hii, msimchague Museveni katika uchaguzi mkuu wa 2021,” akasema.

Mtumiaji mwingine wa Twitter Bireete Sarah alisema: “ Museveni ambaye amekuwa mamlakani kwa miaka 34 amejionea mwenyewe umasikini alioletea Waganda.”