Kimataifa

Museveni amsaka kichuna aliyembusu pichani

November 21st, 2018 1 min read

Na PETER MBURU

RAIS wa Uganda Yoweri Museveni anamsaka mwanamke mmoja ambaye amepigwa picha akiibusu picha yake katika bango la kampeni.

Mwanamke huyo ambaye jina lake bado halijajulikana alipigwa picha akivalia tisheti, huku akigusisha mdomo wake kwa ule wa Rais Museveni pichani na kuonyesha kamera mgongo.

Baada ya picha hiyo kuanza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii, rais huyo sasa ameagiza mwanamke huyo atafutwe, japo bado hajapatikana.

Kulingana na afisa mmoja wa ngazi ya juu katika chama tawala nchini humo, mwanamke huyo bado anatafutwa japo hajajitokeza.

“Ikiwa yeyote anaweza kumpata mwanamke huyu, tafadhali mfahamishe kuwa Rais anataka kupiga picha naye. Tufajhamisheni ikiwa mnamjua,” akasema Bw Don Wanyama.

Picha hiyo iliashiria furaha ya mwanamke huyo kwa Rais Museveni, kwa wazi ikionyesha kuwa ni mfuasi wake sugu.

Kisa hiki kimetokea wakati uchaguzi wan chi hiyo unanukia, Rais Museveni akitarajia kushindana na aliyekuwa Waziri Mkuu Amama Mbabazi na mpinzani Kiiza Besigye.