Habari Mseto

Museveni amtembelea Rais Mstaafu Daniel Arap Moi

March 30th, 2019 1 min read

Na PETER MBURU

RAIS wa Uganda Yoweri Museveni Ijumaa alimtembelea Rais Mstaafu Daniel Moi nyumbani kwake Kabarnet Gardens, Jijini Nairobi kabla ya kukamilisha ziara yake ya siku tatu nchini.

Baada ya ziara za kikazi maeneo tofauti Mombasa na Nairobi pamoja na Rais Uhuru Kenyatta na maafisa wengine wakuu serikalini, Rais Museveni alitenga muda kukutana na kuzungumza na Mzee Moi, kabla ya kuondoka kuelekea Kampala.

Katika picha iliyochapishwa kwenye ukurasa wa Facebook kwenye akaunti ya seneta wa Baringo Gideon Moi, Rais Museveni, Mzee Moi na seneta Moi wanaonekama wameketi wakishiriki gumzo.

Seneta Moi katika maneno yaliyoandamana na picha hiyo alisema: “Leo (Ijumaa) Rais wa Uganda Yoweri Museveni alimtembelea Rais Mstaafu Mzee nyumbani Kabarnet Gardens. Ziara yake ni ishara ya uhusiano wa ndani ambao wamejenga kwa miaka mingi na nimefurahi kuwa unaendelea hadi leo.”

Kiongozi huyo, hata hivyo, hakufafanua zaidi kuhusu ziara ya Museveni wala walichozungumzia na Mzee Moi.

Baada ya ziara hiyo, Rais Museveni alishiriki hafla ya kuhutubia wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kenyatta, Nairobi ambapo palitokea purukushani baadhi ya wanafunzi kuandamana wakimsifu mwanasiasa kijana nchini Uganda, Robert Kyagulanyi ‘Bobi Wine’.