Museveni angali mbele Bobi Wine akisisitiza wanajeshi walilazimisha raia kupigia kura ‘dikteta’

Museveni angali mbele Bobi Wine akisisitiza wanajeshi walilazimisha raia kupigia kura ‘dikteta’

DAILY MONITOR na CHARLES WASONGA

SHUGHULI za kuhesabu kura Uganda ziliingia siku yake ya pili Jumamosi huku matokeo yasiyo rasmi yakionyesha Rais Yoweri Museveni akiwa angali kifua mbele ya kupata asilimia 69 ya kura zilizopigwa.

Naye mpinzani wake wa karibu, Robert Kyagulanyi, almaarufu Bobi Wine, amepata asilimia 30.91 ya kura hizo.

Kulingana na kifungu cha sita cha matokeo ya muda yaliyotolewa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Uganda (UEC) Jaji Simon Byabakama, katika kituo cha kitaifa cha kujumuisha kura cha Kyambogo jijini Kampala, Museveni alipata kura 4,340,134 milioni huku Bobi Wine anayegombea urais kwa tiketi cya Chama cha National Unity Platform (NUP) alipata kuta 2,164, 347.

Hata hivyo, Bobi Wine mwenye umri wa miaka 38 amepinga matokeo hayo akitaja kama “feki”.

Anadai kuwa Jaji Byabakama amefumbia macho visa vya udanganyifu vilivyotokea katika uchaguzi huo uliofanyika Alhamisi na zilizoendelezwa na maafisa wa usalama.

“Katika maeneo mengine wanajeshi na polisi waliwapa watu karatasi za kura ambazo zilikuwa zimetiwa alama kuonyesha wamempigia Museveni kura. Vile vile, waliwatisha watu na kuwalazimisha kumpigia kura dikteta huyo,” Bobi Wine akasema.

“Tumekusanya ushahidi tosha ambao utawasilishwa kwa wananchi baada ya mawasiliano ya intaneti kurejeshwa kote nchini,” akaongeza.

Hata hivyo, Naibu Msemaji wa Jeshi la Kitaifa Deo Akiiki alipuuzilia mbali madai hayo akitataja kama ya “kueneza chuki.”

“Madai hayo yanalenga kupaka tope jina la Jeshi la Ulinzi Nchini Uganda (UPDF),” akasema.

Bobi Wine, ambaye matokeo yake yanaonyesha aemepata uungwaji mkono katika maeneo ya mashambani, tangu alipoingia ulingo wa siasa, aliwaambia wafuasi wake kwamba amejetolea kumaliza utawala wa miaka 35 wa Rais Museveni.

“Mapambano yetu ndio yameanza na hayatakoma,” aliwaambia wanahabari Ijumaa nyumbani kwake katika kijiji cha Magere, Wilaya ya Wakiso.

Wakati huo huo, mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Jaji Byabakama aliwahakikishia Waganda kuwa watajua Rais wao ndani ya saa 48 kulingana na matakwa ya Katiba ya nchi hiyo.

Kuhusu madai ya Bobi Wine kuhusu kuwepo kwa visa vya udanganyifu, mwenyekiti huyo alimtaka kutoa ushahidi kuonyesha kuwa matokeo yaliyotangazwa hayalandani na fomu zilizotiwa saini na maajenti wake.

You can share this post!

Uhuru atandika Ruto 3-0

Mshtakiwa ajifungia chooni akiogopa kujua hukumu