Kimataifa

Museveni apiga kamari marufuku Uganda kuokoa vijana

January 23rd, 2019 1 min read

MASHIRIKA Na PETER MBURU

RAIS wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni amepiga marufuku uchezaji Kamari wa michezo katika taifa hilo, akiamrisha kuwa leseni za kampuni za kucheza michezo hiyo zifutiliwe baada ya muda wa sasa kukamilika.

Waziri wa mipango ya serikali Uganda David Bahati alisema hivyo Jumanne, akisema kuwa hatua ya Rais huyo ilichochewwa na hali ya kampuni hizo kuwapotosha vijana wengi.

“Tumepokea amri kutoka kwa Rais Museveni kuwa tukome kutoa leseni kwa kampuni za Kamari (yani betting, gamind na gambling). Kutoka sasa hakuna kampuni itakayopewa leseni ya kufanya kazi tena,” akasema Bw Bahati.

Alikuwa akizungumza wakati wa kufungwa kwa kongamano la siku nne ambapo alikuwa akimwakilisha Rais.

Serikali ya nchi hiyo ilisema kuwa kanisa limekuwa likipinga hali ya kampuni hizo kupotosha taifa na kupelekea vijana kutofanya kazi wala kutofanya kitu cha maana na pesa wanazopata.

Msemaji wa wizara ya Fedha Uganda Jim Mugunga alisema kuwa hakuwa na habari kuhusu amri hiyo ya Rais lakini akasema kuwa kwa kuwa ilitolewa na waziri, hakuwa na sababu ya kuitilia shauku.

“Hizo ni haari njema,” akaongeza Bw ugunga.