Museveni atetea kutuma jeshi DRC

Museveni atetea kutuma jeshi DRC

KAMPALA, Uganda

Na DAILY MONITOR

RAIS Yoweri Museveni wa Uganda amejitetea kwa Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) kuhusu hatua yake ya kupeleka majeshi katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kusaka magaidi.

Rais Museveni alikutana na wawakilishi wa UNSC kutoka Amerika, China, Urusi, Ufaransa na Uingereza katika Ikulu ya Entebbe nchini Uganda kujaribu kuwashawishi ni kwa nini alivamia nchi jirani.Museveni aliambia maafisa hao kuwa alialikwa na DRC kutuma majeshi nchini humo kupambana na waasi wa kundi la Allied Democratic Forces (ADF).

Kiongozi huyo alisema kuwa operesheni hiyo inaendeshwa na majeshi ya Uganda kwa ushirikiano na wanajeshi wa DRC na kuwa msako huo unaendelea vyema.Museveni alijitetea kuwa aliamua kutuma majeshi DRC kutokana na hofu kwamba magaidi wa ADF wangeanza kushambulia watu vijijini.

Uganda ilituma wanajeshi wake nchini DCR baada ya washambuliaji wa kujitoa mhanga kulipua mabomu karibu na kituo cha polisi cha Central na majengo ya bunge mwezi uliopita.Kundi la ADF ambalo ni mshirika wa mtandao wa kigaidi wa Islamic State (ISIS), lilikiri kuhusika na mashambulio hayo.

Kundi hilo pia lilihusika na shambulio la bomu kwenye kituo cha mabasi katika barabara ya Kampala-Masaka ambapo watu tisa walifariki mnamo Julai, mwaka huu.Maafisa hao wa UNSC waliunga mkono operehseni hiyo lakini wakataka jeshi la Uganda kushirikiana na kikosi cha UN kinacholinda amani nchini DRC (Monusco) chenye wanajeshi 14,000.

Jumanne, wanajeshi wa Uganda walirusha makombora kwenye eneo linalodaiwa kuwa kambi ya waasi wa ADF mashariki mwa DRC.Katika hotuba yake kwa taifa mwezi uliopita, Museveni alishutumu vikosi vya Monusco kwa kushindwa kuangamiza waasi wa ADF.

Rais Museveni alisema kuwa waasi hao wamekuwa wakikata miti na kuuza mbao nchini DRC bila kudhibitiwa.Balozi wa Uganda katika Umoja wa Mataifa, Adonia Ayebare, aliyehudhuria mkutano huo, alisema kuwa maafisa hao wa UNSC waliagiza Uganda kushirikiana na MONUSCO kuhakikisha kwamba opereheni hiyo inaendeshwa kiungwana bila kudhuru raia wa DRC wasio na hatia.

Kikosi cha MONUSCO, hata hivyo, jana kilisema kuwa hakitajiunga na wanajeshi wa Uganda na DRC kupambana na waasi wa ADF. Badala yake, Monusco walisema watawasaidia kuhakikisha kuwa hawaumizi raia wasio na hatia.

Msemaji wa MONUSCO, Mathias Gillman, alisema kuwa vikosi hivyo, vimezuiliwa kushiriki kwenye operesheni za mirengo.UN inatarajiwa kuanza kuondoa vikosi vya MONUSCO nchini DRC kuanzia Disemba 20, mwaka huu, kwa mujibu wa mkataba uliotiwa saini mwaka jana.

Uganda imekuwa ikishinikiza vikosi vya MONUSCO kujiunga nao katika kupambana na magaidi wa ADF.Hatua ya serikali ya Uganda kutuma majeshi yake DRC imeshutumiwa vikali na viongozi wa upinzani ambao wanasema kuwa ni haramu.

Aliyekuwa mwaniaji wa urais Robert Kyagulanyi anasema kuwa Museveni alipeleka majeshi nchini Uganda bila kuidhinishwa na bunge.

You can share this post!

Merkel ang’atuka baada ya kuongoza Ujerumani miaka 16

Mama kortini kukiri kuua mwanawe

T L