Museveni atuma jeshi kumzima Bobi Wine

Museveni atuma jeshi kumzima Bobi Wine

Na DAILY MONITOR

KAMPALA, Uganda

POLISI na jeshi jana Jumanne walizunguka makazi ya mwanasiasa Bobi Wine na kumzuia kufanya ziara katika wilaya ya Kayunga, alikotarajiwa kumfanyia kampeni mwaniaji ubunge wa chama chake katika wilaya hiyo.

Vikosi vya usalama viliweka vizuizi vya barabarani karibu na makazi ya Wine, yaliyo katika eneo la Magere, wilaya ya Wakiso. Wine ndiye kiongozi wa chama cha National Unity Platform (NUP).

“Leo asubuhi, jeshi na polisi waliingia katika makazi yangu usiku wa manane na kuyazunguka kila mahali. Nilikuwa nimepanga kwenda katika wilaya ya Kayunga kukifanyia kampeni chama chetu. Hicho ni kitendo kinachoonyesha serikali inaogopa kushindwa tena,” akasema Wine, kwenye ujumbe alioweka katika mtandao wa Twitter.

Mbunge wa Makindye Mashariki, Derrick Nyeko, ni miongoni mwa watu waliozuiwa kufika kazika makazi hayo.

Baadaye, Wine alisema kuwa polisi walimkamata mmoja wa walinzi na wafanyakazi wake.

“Serikali imetuma kikosi kikubwa cha wanajeshi kuzunguka makazi yangu. Hakuna yeyote anayeruhusiwa kuingia ama kutoka. Mlinzi wetu mmoja na mfanyakazi wa nyumbani wamepigwa, kuhangaishwa na hatimaye kukamatwa kwa njia ya kikatili. Vile vile, wamenyang’anywa simu zao. Hatutaendelea kuvumilia ukatili huu wa serikali. Huwa (Museveni) ananiweka katika kizuizi cha nyumba na baadaye kutumia fedha za umma kuwasafirisha watu katika wilaya ya Kayunga kumshangilia. Hatutapumzika hadi tuikomboe nchi yetu,” akasema muda mfupi baada ya gari la polisi kuingia katika makazi yake.

Uwepo wa maafisa hao ulijiri saa chache baada ya Mkuu wa Wilaya ya Kayunga, Ssempala Kigozi kusema kuwa Wine hangekubaliwa kuzuru wilaya hiyo kumfanyia kampeni Harriet Nakwedde, anayewania ubunge kwa tiketi ya NUP.

Kampeni hizo zimeisha rasmi leo Jumatano.

Hata hivyo, msemaji wa polisi, Fred Enaga, alipuuzilia mbali madai ya mwanasiasa huyo.

“Hakuna yeyote ambaye amemzuia Bobi Wine kukifanyia kampeni chama chake katika wilaya ya Kayunga. Hata hivyo, Tume ya Uchaguzi (EC) ilitoa masharti yanayopaswa kuzingatiwa ili kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.”

Jumanne, magari ya polisi yaliyojihami yalionekana yakipiga doria katika wilaya hiyo, saa chache kabla ya Rais Museveni kuwasili. Rais Museveni alitarajiwa kumfanyia kampeni Andrew Muwonge, anayewania nafasi hiyo kwa tiketi ya chama tawala cha National Resistance Movement (NRM).

Rais Museveni alitarajiwa kufanya mikutano miwili ya kampeni- katika maeneo ya Kayonza na Basaana.

Mabasi ya chama cha NRM yalionekana yakiwasafirisha wafuasi wa Rais Museveni katika maeneo hayo.

Vikosi vya usalama vimekuwa vikimlaumu Wine kwa kutoshirikiana navyo.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa NUP, Lewis Rubongoya, alisisitiza kuwa Wine ana haki ya kufanya mkutano mahali popote pale bila kuziarifu idara za usalama.

“Tumesikia onyo ambazo tumepewa na polisi. Hata hivyo, lazima chama chetu kiendelee na kampeni zake kama ilivyopangwa,” akasema Rubongonya.

Mwenyekiti wa NUP katika wilaya hiyo, Ben Ojambo, alisema wataendesha kampeni zao kwa kuzingatia kanuni na masharti yote yaliyowekwa.

“Sisi huwa tunazingatia na kufuata sheria. Hatujui sababu ya polisi kuanza kutuhangaisha kama uchaguzi uliopita,” akasema Ojambo.

Wadadisi wanasema uchaguzi huo ni muhimu kwa Rais Museveni, baada ya baadhi ya mawaziri wake kushindwa kutetea viti vyao vya ubunge kwenye uchaguzi uliofanyika Januari.

“Ikizingatiwa Rais Museveni analenga kuendeleza utawala wake, yuko tayari kufanya lolote kujifufua upya kisiasa baada ya washirika wengi wake wa kisiasa kushindwa kwenye uchaguzi wa Januari,” akasema Prof Phanice Musambo, ambaye ni mhadhiri wa siasa katika Chuo Kikuu cha Makerere.

You can share this post!

NJENJE: Matumizi ya pesa kwa njia ya simu yaongezeka

Korti yaondoa agizo la Kinoti kutupwa jela

T L