HabariSiasa

Musila aanika siri za Kalonzo

March 24th, 2019 2 min read

Na MWANDISHI WETU

ALIYEKUWA mwenyekiti wa chama cha Wiper, David Musila, amemuumbua kiongozi wa chama hicho, Kalonzo Musyoka, akionyesha jinsi alivyomsaliti licha ya kumsaidia kisiasa baada ya kukosana na Rais mstaafu Daniel Moi mnamo 2002.

Katika kitabu chake kipya, Seasons of Hope, Bw Musila anaelezea jinsi alivyomsaidia Kalonzo kuwa makamu wa rais katika iliyokuwa serikali ya muungano, kuchangisha pesa za kampeni katika mataifa mbalimbali na kumwezesha kuteuliwa mgombeaji mwenza wa Raila Odinga kwenye uchaguzi mkuu wa 2013.

“Alipogura KANU na kujiunga na chama cha LDP, nilisimama naye hata wakati ambapo mambo hayakuwa yanamwendea vizuri. Ilinibidi nidanganye kwa manufaa yake katika mkutano wa kisiasa katika shule ya msingi ya Odiado, eneo bunge la Funyula karibu na nyumbani kwa aliyekuwa Makamum wa Rais Moody Awori, wakati wanasiasa waliokuwa waaminifu kwa Rais Daniel Moi walikuwa wanahamia upinzani,” anasema.

“Kalonzo alikuwa anajivuta kuondoka Kanu ili asionekane kumkosea Moi. Ndio maana ilinibidi nisafiri hadi Funyula bila Kalonzo kufahamu kuambia mkutano huo kwamba Kalonzo alikuwa pamoja nao na yeye pia angehama Kanu na kujiunga na upinzani,” anasema huku akieleza kuwa ni yeye aliyeamua kumkabili Kalonzo na kumshawishi kujiuzulu ili “wenzake wasimchukulie kuwa msaliti”.

Musila ambaye ni seneta wa zamani wa Kitui pia anasema, ni yeye na aliyekuwa Seneta wa Machakos Johnstone Muthama ambao mnamo 2008, walishiriki mazungumzo yaliyomwezesha Kalonzo kuteuliwa na Rais mstaafu Mwai Kibaki kuwa Makamu wa Rais baada ya Bw Odinga kupinga ushindi wa rais huyo katika uchaguzi mkuu wa 2007.

“Vile vile, nilimsaidia Kalonzo alipokosana na Uhuru Kenyatta na William Ruto kuelekea uchaguzi mkuu wa 2013. Kalonzo alikuwa amesisitiza kuwa mgombeaji urais wa muungamo wa vyama vya TNA na URP, lakini Uhuru na Ruto walikataa. Badala yake, alipewa kiti cha Kiongozi wa Wengi Bungeni ambacho alikataa,” Bw Musila anasema.

“Baada ya hapo, nilishirikiana na Mheshimiwa Dalmas Otieno na tulifaulu kumshawishi Raila Odinga kumkubali Kalonzo kuwa mgombeaji mwenza wake. Mazungumzo hayo yalifanyika nyumbani kwangu,” anafichua.

Dharau

Lakini licha ya usaidizi huo, Kalonzo alimuonyesha dharau wakati mmoja walipoenda katika taifa moja la Kiarabu (ambalo hajalitaja) kusaka pesa za kampeni.

“Tuliruhusiwa kuingia ndani kukutana na afisa wa wizara ya mashauri ya kigeni. Baada ya mazungumzo mafupi, nilishauriwa kuondoka ili nimsubiri katika chumba kingine. Sikuuliza kiwango cha pesa alichopewa na hakunitobolea siri hiyo,” Bw Musila anasema.

Hali ilikuwa ni hiyo hiyo alipoandamana na Kalonzo katika taifa moja la Afrika Mashariki kuchanga fedha lakini kiongozi huyo wa Wiper akadinda kumfichulia ni pesa ngapi alipewa.

“Mpaka sasa, bado naficha siri zake nyingi japo tumekosana,” anasema. Bw Musila anasema yeye na Kalonzo walianza kutofautiana, kabla ya kubuniwa kwa muungano wa upinzani, NASA na wakati alikuwa akijitahidi kuhakikisha kuwa Raila na Kalonzo wanakubaliana kuhusu ni nani kati yao angekuwa mgombeaji mwenza wa mwenzake.

“Niliandaa mkutano wa wawili hao nyumbani kwangu, ambao pia ulihudhuriwa na kakake Raila, Oburu Oginga. Baada ya mkutano huo, Kalonzo aliwaambia marafiki wake kwamba katika mkutano huo, nilionekana kumpendelea Raila. Kwamba hakuniamini kama mpatanishi,” anasema

Baadaye, Musila anasema, naibu mwenyekiti wa Wiper, Martin Ole Kamwaro, alipendekeza katika mkutano mwingine ulioandaliwa Maanzoni Lodge kuwa Kalonzo akubali kuwa mgombea mwenza wa Raila, kulingana na mwafaka uliokuwa wa muungano wa CORD.

“Kalonzo alikemea Ole Kamwaro na kumfurusha kutoka kamati ambayo ilikuwa ikijadili suala hilo,” asema.

Na siku chache baadaye, Bw Musila alikutana na Muthama mjini Kitui na kumfahamisha aliondolewa katika kamati ya upatanishi na nafasi yake kupewa marehemu Francis Nyenze. ? Hatimaye uhusiano kati ya Musila na Kalonzo ulikatika kabisa miezi michache kuelekea uchaguzi mkuu wa 2017 alipoamua kuwania kiti cha Ugavana wa Kitui dhidi ya Gavana Dkt Julius Malombe.

Lakini licha ya kiongozi huyo wa Wiper kumhakikishia angemuunga mkono, alibadili msimamo dakika za mwisho na kuamua kumuunga mkono Dkt Malombe.