Makala

MUTANU: Juhudi zifanywe kukabili mabadiliko ya hali ya anga

April 25th, 2019 2 min read

Na BERNARDINE MUTANU

MVUA imeanza kunyesha na wakulima huenda wamepata afueni. Wafugaji wa mifugo nao wamefurahi kwani angalau mifugo itapata malisho na maji.

Lakini, Kenya ni nchi inayoshangaza. Kunapokuwa na kiangazi, mamilioni ya watu huumia, na inapokuja mvua, watu pia huumia.

Kwa muda mrefu, wananchi walikuwa wakitarajia mvua ili wapande. Lakini mvua ilichelewa kunyesha na wakulima wakapata hasara zaidi hasa kwa sababu walikuwa wamepanda ila mimea yao ikakauka au mbegu zikaoza.

Hivi sasa, wakulima wanalenga kupanda tena baada ya mvua kuanza kunyesha maeneo mbali mbali. Lakini huenda zoezi hilo lisifanikiwe kwani mvua inatarajiwa kunyesha kwa muda wa majuma mawili yajayo.

Na kama kawaida, tutaingia tena katika kiangazi, ukame na njaa. Imekuwa hivyo tangu jadi licha ya taifa kuwa na uwezo wa kuweka mikakati ya kuzuia hali kuwa mbaya zaidi.

Serikali imekuwa ikitangaza azimio la kutengeneza mabwawa ya maji kwa lengo la kuhakikisha kuwa kuna maji ya kutosha kwa watu na mifugo. Maji pia ni muhimu zaidi kwa wanaofanya kilimo.

Lakini imekuwa ni maneno tu licha ya kuwa maji ya mvua yanazidi kupotea. Israeli ni taifa kame, lakini taifa hilo huuza mazao yake nje ya nchi.

Ingawa mabadiliko ya hali ya anga yanalaumiwa kwa kiangazi na ukame nchini, kuna njia nyingi za kudhibiti athari za mabadilikohaya.

Kwanza, watu wanafaa kutumia msimu wa mvua kupanda miti. Hali tunayoshuhudia nchini na kwingineko imetokana na ukataji miti na uharibifu wa mazingira. Ni hali inayoweza kurekebishwa ingawa kinachohitajika ni hatua ya pamoja, inayohusisha Kenya na ulimwengu kwa jumla.

Pia, msimu wa mvua ni wakati wa kuteka maji ili kuweza kuyatumia wakati wa ukame. Lakini hakuna mabwawa na maji yote ya mvua kama kawaida yatapotea tu halafu tuanze kulia tena.

Wakati wa kiangazi kwa upande wake ni wakati wa kuchimba mabwawa au kutengeneza miradi ya unyunyiziaji. Lakini kwa sasa inaonekana mabadiliko ya hali ya hewa sio suala lililopewa kipaumbele.

Hata hivyo, ukweli ni kwamba, bila kuwa na chakula cha kutosha, itakuwa vigumu sana kwa taifa hili kuendelea. Hii ni kutokana na kuwa watu watatumia pesa nyingi kununua chakula na hawatakuwa na pesa zaidi za kujiendeleza.

Hivyo, masuala yote yanayoathiri uwepo wa chakula nchini yanafaa kupewa kuangaziwa kwa umuhimu mkuu. Mabadiliko ya hali ya anga yapo na yataendelea kuwa lakini athari zake zinaweza kudhibitiwa.

Ni suala ambalo halifai kufumbiwa macho zaidi kuliko ilivyo kwani hivi karibuni janga kubwa la njaa litashuhudiwa ikiwa hakuna hatua muhimu zitakazochukuliwa.

Cha kushangaza ni kuwa tumezoea kuyachukulia masuala kwa umuhimu yanapokuwa ya dharura. Wakati ni sasa na kama sio sasa, ni sasa hivi.