Makala

MUTANU: Serikali isilegeze kamba katika uhifadhi wa misitu

March 7th, 2019 2 min read

Na BERNARDINE MUTANU

VIWANGO vya joto vimezidi nchini na vitaendelea kushuhudiwa nchini hadi mvua ya masika ianze kunyesha.

Lakini sio mara ya kwanza kwa joto jingi kushuhudiwa nchini, katika muda wa miongo kadhaa, joto linazidi kuwa jingi.

Kwa watu wengi wasio na ufahamu, hali hiyo imesababishwa na jua ambalo kwao ‘limekaribia’. Lakini jua halijakaribia, joto jingi limetokana na ongezeko la gesi ambazo zimeziba anga.

Gesi hizo zimetokana na shughuli za kibinadamu hasa ukuaji wa viwanda na samadi ya mifugo ambayo hutoa gesi za joto.

Huku ikiwa vigumu kupunguza viwango vya joto ulimwengu, uharibifu wa mazingira unazidi kuwa na madhara mabaya kwa binadamu na wanyama wa pori.

Kwa mfano, joto jingi nchini limekausha mito ambayo ni muhimu sana kwa maji ya matumizi ya binadamu na wanyamapori.

Kukauka kwa Mto wa Mara, ambao ni muhimu kwa Mbuga ya Wanyamapori ya Mara na Serengeti ni tishio kubwa kwa mbuga hizo na huenda kukasababisha hasara kubwa kutokana na vifo vya wanyama.

Tunajua kuwa mbuga za wanyamapori ni muhimu kwa uchumi wa Kenya kutokana na utalii nchini.

Lakini sio tu mabadiliko ya hali ya anga yanaathiri sekta ya utalii pekee, sekta zingine kama vile ile ya kawi, kilimo na afya zitaathiriwa.

Hii ni kutokana na kuwa, viwango vya maji vinapopungua husababisha uzalishaji wa kawi kwenda chini, kilimo kupungua na magonjwa yanayotokana na maji kama kipindupindu kuongezeka.

Hii ni kumaanisha kuwa serikali inafaa kujiandaa vilivyo kukabiliana na mabadiliko ya anga kwa sababu athari zake ni kubwa.

Athari zake zimeanza kuonekana kwani kumekuwa na kiangazi mara kwa mara ambacho kimefanya watu wengi kuathiriwa na njaa. Vile vile, kila msimu wa mvua, kumekuwa na milipuko ya magonjwa kama vile kipindupindu, dengue, malaria na magonjwa mengine.

Ingawa serikali peke yake haiwezi kurekebisha hali, mashirika yanafaa kuungana ili kuelimisha umma kuhusu jinsi ya kukabiliana na mabadiliko hayo.

Kwa mfano, wananchi wanafaa kufunzwa umuhimu wa kuhifadhi misitu na vyanzo vya maji kama vile msitu wa Mau ambao ni mnara wa maji na uhai wa Mbuga za Wanyamapori za Mara na Serengeti.

Ingawa kumekuwa na miradi ya unyunyiziaji nchini, bado idadi kubwa ya wananchi hawanufaiki kutokana na miradi hiyo.

Wananchi wanafaa kufunzwa jinsi ya kufanya kilimo cha maji hata kwa viwango vidogo kwa kuvuna maji wakati wa mvua na kuyatumia kupanda mimea wakati wa kiangazi.

Ingawa jamii za wafugaji zinathamini sana mifugo wao, wanafaa kuelezwa manufaa ya kufuga wachache ili kukabiliana vyema na kiangazi na pia gesi ya ‘methane’ ambayo ni moja ya gesi za joto ambazo zimeendelea kuyeyusha barafu ulimwenguni na kusababisha mabadiliko ya hali ya hewa.

Serikali haifai kulegea katika kampeni ya kuhifadhi Msitu wa Mau na misitu mingine nchini kwani pasi hilo, wananchi watakabiliwa na changamoto zaidi miaka kadhaa kuanzia leo.