Makala

MUTANU: Serikali itilie maanani kansa katika bajeti ya 2019/2020

March 14th, 2019 2 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Mbunge wa Kibra Ken Okoth amejitokeza wazi na kutangaza kuwa anaugua kansa. Licha ya watu wengi kumwonea huruma, ni mmoja kati ya watu wakakamavu zaidi kwani ni wachache sana wanaoweza kuchukua hatua kama hiyo.

Nchini, ugonjwa wa kansa umekuwa ni changamoto kubwa na ninaungana na wote wanaosema kwamba kansa inafaa kutangazwa janga la kitaifa.

Ni ugonjwa ambao unagharimu pesa nyingi kutibu na nyakati nyingi huwa ni vigumu kutibika zaidi ya kuwa huwafanya waathiriwa kuwa dhaifu sana na kuwaacha wengi maskini.

Bw Okoth, amekuwa sura ya kansa nchini; ni wakati wa serikali kuchukua hatua zifaazo kukabiliana na kansa kwani sio watu wengi wanaoweza kumudu matibabu ya ugonjwa huo.

Idadi kubwa ya wananchi hutafuta tiba nje ya nchi hasa India, hatua ghali sana, kwa kukosa matibabu muafaka nchini.

Ingawa baadhi yao wanaweza kujigharamia awamu kadhaa za matibabu, mara nyingi hubidi familia kutafuta fedha zaidi kutoka kwingineko au kufanya harambee kugharimia matibabu hayo.

Zaidi ya kuwa kansa ni ghali kutibu, nchini Kenya kuna wataalam wachache tu wa kukabiliana na ugonjwa huo zaidi ya kuwa hospitali ni chache tu zinazotibu kansa nchini.

Huku serikali ikitarajiwa kutangaza bajeti ya mwaka wa kifedha wa 2019/2020, baadhi ya sekta zinazofaa kutiliwa maanani zaidi ni afya.

Matibabu ya kansa yanafaa kutiliwa maanani zaidi kwani imekuwa vigumu sana kudhibiti ugonjwa huo ambao haubagui kwani wazee kwa vijana, matajiri kwa maskini, wake kwa waume wote wameathiriwa kwa njia moja au nyingine.

Serikali inafaa kununua mashine zaidi, kujenga hospitali zaidi na pia kupunguza bei za dawa za kutibu kansa zaidi ya kusomesha na kuajiri wataalam zaidi.

Huku idadi ya waliogua kansa ikizidi kuongezeka, labda ni wakati wa serikali kuimarisha ufadhili katika utafiti kuhusiana na kiini cha kansa.

Pia, wananchi wanahitaji kuelimishwa kuhusiana na kansa na magonjwa mengine na jinsi wanavyoweza kujikinga

Ni vigumu sana kwa taifa kukua ikiwa watu wake ni wagonjwa au wadhaifu. Bw Okoth ni mmoja wa wabunge wa umri mdogo ambao wamewafanyia kazi wananchi.

Inavunja moyo kumwona akiwa katika hali hiyo na wengi wamekuwa wakijiuliza maswali kuhusiana na hali yake.

Nchini Kenya, watu 90 hufa kila siku kwa sababu ya kansa kulingana na utafiti. Kila mwaka, vifo vinavyotokana na kansa vimekadiriwa kuwa zaidi ya 30,000.

Haifai kansa kuzamisha matumaini ya wananchi kwani idadi kubwa ya wanaoaga dunia inahofisha hasa kutokana na kuwa matibabu ya kansa huacha familia nyingi maskini.

Ni wakati wa kuchukua hatua madhubuti kwani changamoto zinazoletwa na kansa ni nyingi ikiwemo ni pamoja na athari katika familia na kazini pamoja na uwezo mkubwa wa watoto kuachwa na baba au mama au familia kupoteza watu wanaoikimu familia.