Makala

MUTANU: Serikali izingatie maisha ya mwananchi wa kawaida 2019

December 27th, 2018 2 min read

Na BERNARDINE MUTANU

MSIMU wa sikukuu unakaribia kukamilika na siku kadhaa zijazo, wanafunzi wanatarajiwa kurejea shuleni kwa muhula wa kwanza 2019.

Ni wakati wa kuanza mwaka mwingine na matarajio mapya, mambo mapya na mwamko mpya.

Kila mwaka mpya unapoanza, watu huwa na matumaini makubwa kwamba mambo yatakuwa tofauti ikilinganishwa na mwaka uliokamilika.

Hata hivyo, kila unapodhania mambo yamebadilika ndivyo husalia vile vile. Bili, madeni, ushuru, yote yanasalia vile vile.

Huku gharama ya maisha ikiwa imepanda sana hasa kutokana na ongezeko la bei za bidhaa, wananchi wanatumainia kuwa baadhi ya gharama zitapungua ili kuwarahisishia mzigo.

Maelfu ya wazazi watapeleka watoto wao katika kidato cha kwanza na gharama yake inatarajiwa kuwa ya juu sana kwani mbali na karo, wazazi wanatarajiwa kununua vitabu na vitu vingine vya matumizi shuleni.

Hivyo, ni matumaini ya kila mmoja kwamba serikali itarahisisha mambo 2019. Mwaka wa 2018 ulikuwa mgumu na mchungu sana hasa kwa wananchi wa kawaida, wengi wasio na kazi.

Hii ni kutokana na mambo mbali mbali ikiwemo ushuru takriban kwa kila kitu na ukosefu wa ajira huku baadhi ya kampuni zikiwa zimepunguza wafanyikazi kutokana na hali ngumu ya kibiashara.

Ukweli ni kwamba wananchi wengi hawakusherehekea Krismasi vyema kwa sababu ya changamoto za kifedha. Kulingana na Mamlaka ya Kukusanya Ushuru nchini (KRA), ‘kulipa ushuru ni kujitegemea’. Ninakubaliana kabisa na kauli hiyo kwa sababu lazima taifa lisonge mbele.

Hata hivyo, ni vyema serikali kuwajali wananchi wasio na mapato ya juu kwani wengi wanataabika; wengi hawawezi kununua vitu vya kimsingi na ukweli ni kwamba hawatukuwa na uwezo wa kuwapeleka watoto wao wanaojiunga na kidato cha kwanza shuleni.

Huenda watoto wengi wakakosa nafasi katika shule za kitaifa kwa sababu wazazi hawana uwezo.

Ni kwa kuzingatia hili ambapo serikali inafaa kukabiliana na hali mwakani ili kuhakikisha wananchi wana ajira na uwezo wa kujitegemea na kuendeleza taifa.

Taifa haliwezi kuendelea ikiwa zaidi ya nusu ya wananchi wanaishi chini ya dola kwa siku.

Matumaini yangu ni kuwa 2019 wananchi watashuhudia mabadiliko ya kweli.