Makala

MUTANU: Wazazi wasipowaelekeza watoto, upotovu utazidi

June 5th, 2019 2 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Kilikuwa kisa cha kushangaza kwa vijana wa umri mdogo walipomteka nyara na kumuua mvulana wa umri mdogo mbali na kuitisha fidia kutoka kwa wazazi wake ili wamwachilie.

Hiyo ni taswira kamili ya jamii yetu ilivyo nchini. Uhayawani umewatoka wanyama na kuwaingia binadamu.

Cha kushangaza ni kuwa kisa hicho kilihusisha watoto wa umri mdogo, karibu wote wakiwa wenye umri kati ya miaka 15 na 18.

Ingawa wataadhibiwa kisheria, hilo si suluhisho la kinachoendelea katika jamii na huenda visa kama hivyo vikaendelea kuripotiwa mara kwa mara katika siku zijazo.

Wakati wa sherehe za kuadhimisha Sikukuu ya Madaraka, Rais Uhuru Kenyatta alizungumzia suala la mauaji miongoni mwa wananchi yanayoendelea kuripotiwa kila siku.

Rais alikashifu vikali visa hivyo, zaidi ya kutambua viwango vya juu vya mafadhaiko miongoni mwa wananchi. Visa vya mauaji au kujiua vinatokana na shinikizo za mambo katika jamii.

Ingawa kuna haja kubwa ya kufanya utafiti ili kutambua kiini kamili cha visa hivyo vya kuhuzunisha, ukweli ni kwamba jamii imechangia pakubwa.

Ingawa sitaki kuhukumu, watoto wa umri mdogo kama hao wa Kakamega hawawezi kufanya hivyo bila kuiga kutoka kwa watu wengine au kupata mafunzo.

Aidha, watoto wanaweza kuhusika katika uhalifu kama huo kwa kusukumwa na hali katika jamii au kutazama video au filamu zinazoonyesha uhalifu.

Ukifuatilia zaidi, utapata kuwa watoto kama hao huwa wanachama wa madhehebu ambayo huwapotosha.

Ingawa kuna masuala mengi ambayo huchangia mauaji au hatua ya kujitoa roho, ni vyema wananchi kuelewa kuwa ‘mtoto umleavyo ndivyo akuavyo’.

Watoto wengi hukua wakijua kuwa vurugu ni kawaida, kutusi ni kawaida, kudanganya ni kawaida, kuiba ni kawaida au hata kumchapa mtu ni kawaida. Hii ni kwa sababu hukua wakiona mambo hayo yakifanywa katika jamii na wazazi wao, ndugu zao wakubwa, majirani au hata marafiki.

Wanapokuwa watu wazima, inakuwa ni vigumu kujizuia kuhusika katika mambo kama hayo na ndiposa kuna idadi kubwa ya wafungwa wa umri mdogo nchini.

Ninachosema ni kwamba watoto, ambao ni viongozi au wazazi wa kesho, wamekosa mwelekezi au mtu wanayeweza kumuiga au kuwashauri.

Wazazi wamewafeli watoto wao kwani zaidi ya kuwa hawapatikani tena kuwaelekeza watoto wao kutokana na shughuli za hapa na pale, baadhi yao hawawafunzi maadili na umuhimu wa kuwa waadilifu. Zaidi, baadhi ya wazazi huwa hawawaelekezi watoto wao makanisani, misikitini au mahekaluni ili kupata ‘chakula’ cha kiroho.

Kutokana na hilo, wengi hukua wakiwa watupu kiroho, hivyo, hujipata wamevunjika moyo au kutamauka maishani, kisha kuona heri wafe kwa kujitoa uhai au waondoe uwepo wa mtu au watu walio ‘kikwazo’ katika maisha yao.

Na ndiyo maana kuna visa vingi vya mauaji au kujitoa uhai. Tunachohitaji kwa sasa ni kujirudi kama wazazi na kuchukua hatua za kimsingi katika malezi.