HabariSiasa

Muthama aapa kuzima Kalonzo kisiasa 2022

September 1st, 2020 2 min read

WYCLIFF KIPSANG na GASTONE VALUSI

CHECHE za maneno kati ya kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka na aliyekuwa seneta wa Machakos, Bw Johnston Muthama, zimeongezeka, huku Bw Muthama akiapa kumwonyesha Bw Musyoka kivumbi ifikapo 2022.

Katika mahojiano ya redio jana, Bw Muthama alihoji kuwa hajuti kugura chama cha Wiper na akasisitiza kuendelea kumpigia debe Naibu Rais William Ruto kwa azma yake ya urais mwaka wa 2022.

“Kalonzo anaendeleza chama kama mali yake binafsi. Mwaka wa 2022 atajua hajui. Hii itakuwa mara yake ya mwisho kushindana kisiasa,’ alisema Bw Muthama.

Alihoji kuwa hata kama Dkt Ruto hatapewa tiketi ya kugombea urais na chama cha Jubilee mwaka wa 2022, kuna vyama vingi vya kisiasa anavyoweza kutumia.

Alipuuzilia mbali pia mahasimu wake wanaodai ameungana na Dkt Ruto kwa sababu za kifedha.

“Sitaki hela za Ruto kwani niko na zangu za kunitosha. Maoni yangu tu ni kwamba wakati umefika mtoto wa maskini kuchaguliwa kuwa rais,’ alisema Bw Muthama. 

Juma lililopita, Bw Muthama alitofautiana na Bw Kalonzo baada ya kumsihi kumuunga mkono naibu rais 2022. Bw Musyoka alimwambia Bw Muthama kuwa yeye anaweza kujiamulia kisiasa na mtu yeyote hataongea kwa niaba yake.

Alimlaumu Bw Muthama kwa kutokuwa na shukrani licha ya yeye kumlea kisiasa. Hata hivyo, Bw Muthama jana alidai kuwa ni yeye ambaye amemsaidia Bw Kalonzo akihoji kuwa yeye alikuwa miongoni mwa viongozi waliomwongelesha aliyekuwa rais Mwai Kibaki kumteua kama makamu wa rais mwaka wa 2002.

Baadhi ya wanasiasa wa eneo la Ukambani wameonya kuwa mizozo hiyo ya viongozi wa eneo hilo ni hatari kwa maazimio yao ya kuwa na nafasi bora katika uongozi wa taifa.

Mbunge wa Matungulu, Bw Stephen Mule, jana aliwataka viongozi wa Ukambani kushirikiana ili kuimarisha umoja wa wakazi ndipo waongee kwa sauti moja katika uchaguzi mkuu wa 2022.

Bw Mule alisema kuwa viongozi ni lazima wakome kutusiana kwa kuwa inaaibisha eneo hilo.

Alisema hali ya viongozi kutusiana kila mara kunaonyesha kuwa hawajakomaa na hawawezi kujadili maswala muhimu ya kitaifa. Aliongeza kuwa mizozo hiyo imeathiri maendeleo ya Ukambani.

“Wanachotaka wakazi si kuambiwa watakayempigia kura mwaka wa 2022 bali ni nani atakayeweza kuwahudumia ipasavyo kabla ya uchaguzi ujao,” akasema.

Alisema hayo alipokuwa akikagua Mbunge huyo alipokuwa akikagua mradi wa CDF katika lokesheni ya Katwanyaa, eneo Bunge la Matungulu.