Muthama akwepa tena kampeni za Ruto Machakos kwa sababu ya Gavana Mutua

Muthama akwepa tena kampeni za Ruto Machakos kwa sababu ya Gavana Mutua

PIUS MAUNDU na CHARLES WASONGA

KWA mara nyingine, mwenyekti wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) Johnson Muthama, Ijumaa alikwepa mkutano wa kampeni ulioongozwa na Naibu Rais William Ruto katika kaunti ya Machakos.

Hatua hiyo inafasiriwa kuashiria kuwa uhasama kati yake na Gavana wa Machakos Alfred Mutua umezidi kufuatia hatua ya gavana huyo kujiunga na kambi ya Dkt Ruto wiki mbili zilizopita.

Mnamo Ijumaa Dkt Ruto, Dkt Mutua na wabunge Victor Munyaka (Machakos Mjini), Vincent Musyoka (Mwaka) waliungana kumshinikiza kiongozi wa Wiper kugura Azimio la Umoja-One Kenya na kujiunga na Kenya Kwanza (KKA).

Viongozi hao waliojumuisha mgombea mwenza wa Dkt Ruto, Rigathi Gachagua na Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria walimtaka Bw Musyoka kuunga mkono azma ya urais ya Naibu Rais.

Wakati huo, Bw Muthama alikuwa akiendesha kampeni zake katika eneobunge la Matungulu ambapo alipigia debe azma yake ya ugavana.

Aidha, aliwarai wakazi waelekeze kura za urais kwenye kapu la Dkt Ruto ambaye anaungwa mkono na vyama 13 chini ya muungano wa KKA.

“Ukweli usemwe, siwezi kulinganishwa na wanasiasa kama vile Wavinya Ndeti, Nzioka Waita na Francis Maliti. Mimi Muthama ndiye ninafaa zaidi kuwa Gavana wa kaunti ya Machakos,” Bw Muthama akasema.

Vile vile, alimshutumu vikali Dkt Mutua kwa kile alichotaja kuwa usimamizi mbaya wa kaunti ya Machakos.

Bw Muthama ambaye alikuwa ameandamana na mgombea mwenza wake Faith Muli, pia alivumisha mfumo wa kuimarisha uchumi kuanzia mashinani, “bottom-up” .

Aliitaka jamii ya Wakamba kuunga mkono Dkt Ruto kwa sababu yeye ndiye yuko katika nafasi bora ya kumrithi Rais Uhuru Kenyatta.

Bw Muthama alitoa wito kwa wakazi wa Machakos kupigia kura wawaniaji wa UDA pekee kuanzia viti vya udiwani hadi urais.

Kauli hiyo pia inaendeleza uhasama kati yake na Dkt Mutua ambaye anapaswa kushirikiana naye kuendeleza kampeni za Dkt Ruto katika eneo pana la Ukambani.

Mmoja wa wapinzani wa Muthama katika kinyang’anyiro cha ugavana ni Bw Maliti ambaye ni naibu wa Dkt Mutua. Bw Maliti anawania kiti hicho kwa tiketi ya chama cha Maendeleo Chap Chap (MCC) kinachoongozwa na Dkt Mutua.

Uchunguzi wa Taifa Leo umebaini kuwa Bw Maliti ameweka nembo ya muungano wa Kenya Kwanza katika baadhi ya mabango yake na kuondoa nembo ya Azimio la Umoja.

Hii ni kufuatia hatua ya Dkt Mutua kutangaza kuwa amejiondoa kutoka Azimio na kujiunga na Kenya Kwanza unaoongozwa na Dkt Ruto.

Kando na Muthama, Mbunge wa Machakos Mjini Victor Munyaka pia hajafurahishwa na hatua ya Dkt Mutua kujiunga na kambi ya Naibu Rais.

Bw Munyaka anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa mwaniaji kiti hicho kwa tiketi ya MCC Bw Caleb Mutiso.

  • Tags

You can share this post!

Kevin de Bruyne na Phil Foden washinda tuzo za Mchezaji...

Timbe atwaa Kombe la FA Thailand

T L