Muthama na Koech wataka walipwe fidia baada ya kukamatwa

Muthama na Koech wataka walipwe fidia baada ya kukamatwa

Na PHILIP MUYANGA

ALIYEKUWA Seneta wa Machakos, Bw Johnstone Muthama na mbunge wa Belgut, Bw Nelson Koech, wanataka kulipwa fidia baada ya kukamatwa na polisi wakati wa uchaguzi mdogo wa eneobunge la Msambweni, Desemba 15.

Viongozi hao wawili wanadai walikamatwa na kuzuiliwa bila taratibu zifaazo kuzingatiwa, jambo ambalo ni ukiukaji wa haki zao za msingi.

Kwenye kesi ambayo wamewasilisha katika Mahakama Kuu ya Mombasa, wawili hao wanataka kukamatwa kwao, kuzuiliwa na nia ya kutaka kuwafungulia mashtaka kutangazwa kama matumizi mabaya ya sheria.

Wanataka hilo pia kutajwa kama ukiukaji wa haki ya malalamishi yao kutosikilizwa. Wawili hao, ambao wamemshtaki Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI), Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma (DPP) na mkuu wa Kituo cha Polisi cha Diani, wanasema wakati wa uchaguzi huo, walikuwa wakimfanyia kampeni Bw Feisal Bader.

Wanashikilia kuwa vitendo hivyo vyote ni ukiukaji wa taratibu zinazopaswa kuzingatiwa na mahakama.Kupitia wakili Gikandi Ngibuini, wanasema Mahakama Kuu ina mamlaka ya kusimamisha mpango wowote wa kuwafungulia mashtaka, ikiwa utakiuka haki zao.

Wanasema kuwa washtakiwa wamevunja katiba kwa kukataa kuwaarifu sababu za kukamatwa na kuzuiliwa kwao.

Vile vile, wanawalaumu polisi kwa kuwanyima nafasi ya kuwasiliana na wakili na watu ambao wangewasaidia walipokuwa kwenye seli.

“Washtakiwa walivunja Sehemu 49 (g) ya Katiba kwa kukosa kufika mahakamani, kuwashtaki au kuuwafahamisha walalamishi sababu ya kukamatwa kwao,” wakaeleza kwenye stakabadhi hizo.

Bw Muthama anasema wakati aliwataka polisi kueleza sababu ya kukamatwa kwake, walimweka kwenye gari lao kwa nguvu na kumpeleka katika kituo cha polisi.

You can share this post!

Tupatane mahakamani, Dorcas Mwende amwambia mamaye Jackline...

Sh19 bilioni za mpango wa elimu bila malipo kutolewa kabla...