Kimataifa

Mutharika kwenye mtihani Malawi ikichagua Rais

May 19th, 2019 2 min read

NA MASHIRIKA

WAPIGAKURA nchini Malawi Jumanne wanatarajiwa kuingia debeni na kumchagua Rais mpya huku ushindani mkali ukitarajiwa kati ya Rais Peter Mutharika na aliyekuwa Makamu wa Rais Saulos Chilima.

Wananchi wa taifa hilo pia watawachagua wabunge na madiwani wa manispaa mbalimbali nchini humo.

Rais Mutharika, 78 ambaye alitwaa uongozi wa taifa hilo mwaka wa 2014, miaka miwili baada ya kifo cha nduguye Rais Bingu wa Mutharika, anatarajiwa kuwa na wakati mgumu kutetea kiti chake kutokana na kile wachanganuzi wanasema ni uongozi mbaya.

Malawi imekuwa ikitegemea sana misaada kutoka mataifa ya uzunguni huku raia wengi wakilalamikia kukithiri kwa visa vya ufisadi ndani ya serikali, visa ambavyo vimelemaza ukuuaji wa uchumi wa taifa hilo.

Kando na ufisadi, utawala wa Rais Mutharika pia umekuwa ukikumbwa na kupotea kwa umeme mara kwa mara, kudorora kwa sekta ya afya na kuongezeka kwa deni la taifa.

Uhasama kati ya Rais Mutharika na Bw Chilima, 46 ulitokota na kufikia kilele chake mwaka jana pale makamu huyo wa zamani wa Rais alipokigura chama tawala cha Democratic Progressive Party(DPP) na kubuni chama chake cha United Transformation Movement(UTM). Rais Mutharika ni wakili maarufu huku mpinzani wake akiwa mtaalamu wa mawasiliano.

Ingawa hivyo, wachanganuzi wamesema kwamba wapigakura vijana ndio watakuwa na sauti kuu katika kuamua mshindi wa uchaguzi huo, ikizingatiwa kwamba wengi wao ndio wamekuwa katika mstari wa mbele kupinga uongozi mbaya na kupanda kwa deni la taifa.

Huku Bw Chilima akihubiri wimbi la mabadiliko kwenye mikutano yake ya kampeni, Rais Mutharika amekuwa akipambana na kusafisha jina lake kuhusu sakata kadhaa za ufisadi ambazo amekuwa akihushishwa nayo.

“Watu hawali siasa. Wanahitaji maendeleo ambayo nimekuwa nikiwaletea na nitaendelea kuwapa nikishinda awamu ya pili,” akasema Rais Jumatano huku akikanusha kwa familia yake ilinufaika na tenda ya kusambaza chakula kwa polisi wote wa taifa hilo.

Kulingana na kiongozi wa wanafunzi Boniface Dulani kutoka Chuo Kikuu cha Malawi, Bw Chilima ana uungwaji mkono kutoka kwa vijana ambao ndio wengi wa wapigakura watakaoshiriki uchaguzi wa kesho.

“Iwapo Bw Chilima atapoteza kwenye uchaguzi huu basi huu utakuwa mwisho wa safari yake ya kisiasa. Iwapo atashinda kutokana na kushabikiwa na vijana wengi, tunatarajia ataleta ufanisi aliokuwa nao kwenye sekta ya kibinafsi ndani ya serikali,” akasema Bw Dulani.