Habari

Muthaura ateuliwa tena kuongoza bodi ya KRA

October 4th, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

ALIYEKUWA Mkuu wa Utumishi wa Umma na Katibu katika Baraza la Mawaziri Francis Muthaura sasa ataendelea kuhudumu kama Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA) hadi Oktoba 21, 2022.

Hii ni baada ya Rais Uhuru Kenyatta kumteua upya kwa wadhifa huo kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia Oktoba 21, 2019, kulingana na tangazo kwenye gazeti rasmi la serikali, toleo la Oktoba 2, 2019.

“Kulingana na mamlaka yanayotokana na sehemu ya 6 (2) (a) ya Sheria ya KRA mie Uhuru Kenyatta, Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi yote Nchini, namteua Francis Muthaura kuwa mwenyekiti wa bodi ya KRA kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia Oktoba 21, 2019,” Rais akasema kwenye tangazo hilo.

Balozi Muthaura, 72, aliteuliwa kwa mara ya kwanza katika wadhifa huo mnamo Mei 23, 2018.

Naibu gavana CBK

Hii ni baada ya Rais Kenyatta kufutilia mbali uteuzi wa aliyekuwa Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Kenya Dkt Edward Sambili ambaye alikuwa akihudumu kama mwenyekiti wa Bodi ya KRA.

Muthaura alihudumu katika serikali ya Rais mstaafu Mwai Kibaki kama Mkuu wa Utumishi wa Umma na Katibu wa Baraza la Mawaziri hadi alipojiuzulu mnamo 2012.

Hii ni baada kukabiliwa na tuhuma za kuchochea na kufadhili ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa 2007 ambapo alifunguliwa mashtaka katika Mahakama ya Kimataifa kuhusu Uhalifu (ICC).

Wengine waliokabiliwa na tuhuma hizo ni Rais Kenyatta, naibu wake William Ruto, aliyekuwa Kamishna wa Polisi Hussein Ali, aliyekuwa Mbunge wa Tinderet Henry Kosgey na Mtangazaji Joshua Arap Sang’.

Balozi Muthaura pia amekuwa akishikilia cheo cha mwenyekiti wa Mamlaka ya Ustawi wa Mshoroba wa Lapsset; mradi wa miundomsingi unaoshirikisha mataifa ya Kenya, Ethiopia na Sudan Kusini.