Mutua aahidi wanandoa ‘zawadi’ ya Sh0.5 milioni wakimchagua rais 2022

Mutua aahidi wanandoa ‘zawadi’ ya Sh0.5 milioni wakimchagua rais 2022

GAVANA Alfred Mutua wa Machakos ameahidi kuwapa wanandoa wapya mkopo wa kati ya Sh500,000 na Sh1 milioni kama ‘zawadi’ ili kuboresha maisha yao, ikiwa atachaguliwa kuwa rais kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2022.

Akizindua manifesto yake ya urais jana jijini Nairobi, Dkt Mutua alisema wanandoa hao watalipa mkopo huo kwa riba ya asilimia 0.5 kwa muda wa miaka 20. “Ni hatua ya kuwawezesha kuboresha maisha ya familia zao,” akasema Dkt Mutua.

Gavana huyo ni miongoni mwa vigogo wa kisiasa wanaoendelea kutangaza azma za kuwania urais kadri uchaguzi huo unapokaribia.Mbali na hayo, Gavana aliahidi kubuni hazina maalum ya chakula kuwasaidia Wakenya ambao wamekuwa wakikumbwa na baa la njaa kutokana na kiangazi katika sehemu mbalimbali nchini.

“Inawezekana kuhakikisha hakuna Mkenya anayefariki kutokana na njaa. Serikali itabuni mpango huo kuhakikisha kila mwananchi anapata chakula cha kutosha,” akasema.Ahadi nyingine alizotoa ni kuboresha maslahi ya vijana, kufufua na kubuni viwanda, afya bora kwa kila Mkenya, kuboresha usalama, sekta ya elimu na kukabiliana na ufisadi.

Dkt Mutua ndiye kiongozi wa chama cha Maendeleo ChapChap, ambacho ndicho atatumia kuwania nafasi hiyo.

You can share this post!

Sharti uchaguzi uwe wa amani -Matiang’i

Kupe wa kisiasa wamfyonza Ruto

T L