Makala

MUTUA: Afrika Kusini iwekewe vikwazo ndio ipate funzo

September 7th, 2019 2 min read

Na DOUGLAS MUTUA

MATAIFA yote yaliyotetea ukombozi wa Afrika Kusini kutoka minyororo ya utawala wa ubaguzi wa rangi yanapaswa kurejea kazini kwa dharura.

Mara hii kibarua kitakuwa kuwakomesha waliofaidi msaada huo wakawa huru kwa maana vitendo na fikra zao zinashabihiana na kichaa cha mbwa.

Kutowakomesha raia weusi wa Afrika Kusini ambao wanawaua weusi wenzao kutoka mataifa mengine yanayoendelea ni kuruhusu ubaguzi sawa na waliopinga enzi zile uendelee.

Raia mweusi wa Afrika Kusini anapaswa kukumbushwa kwa kurejeshwa kwenye nafasi aliyoshikilia duniani hadi miaka ya -90 ili ashike adabu yake sawasawa.

Matatizo ya kiuchumi, ukosefu wa kazi na huduma za kimsingi anazodhani amekosa kutokana na uwepo wa wageni weusi kama yeye nchini mwake yakizidi atapata akili.

Jamii ya kimataifa inapaswa kuungana kuliwekea vikwazo taifa hilo ili vililemaze kikamilifu, dhiki ziwazidie wahuni wanaoua watu kiholela, walilie mkate mkavu wasiupate!

Ni hadi hilo litakapofanyika ambapo tutatatua tatizo la chuki inayoendelezwa na weusi dhidi ya weusi wenzao; kujichukia wenyewe haswa!

Nimesema vikwazo dhidi ya taifa hilo la mwendazake njiwa wa amani, Nelson Mandela, ndivyo vitakavyoleta suluhisho kwa sababu ninaamini viongozi hawafanyi juhudi zozote.

Weusi wanaoitawala nchi hiyo wanapaswa kuzima unyama huo unaoendelezwa na weusi wenzao, lau sivyo tuamini wauaji hao ni mawakala wa watawala.

Ikiwa Rais Cyril Ramaphosa na wenzake katika chama cha African National Congress (ANC) wameshindwa kudhibiti hali, basi vikwazo vitawashinikiza kuondoka madarakani.

Ni rahisi: vikwazo vikiwekwa, vyuma vikaze kabisa kiuchumi, nguvu wanazotumia weusi kuua watu zitaelekezwa kwingine kunakotabirika, yaani kwa viongozi wao.

Kiongozi wa pekee nchini Afrika Kusini aliyeonyesha upendo wa dhati kwa Waafrika wote ni Bw Julius Malema, kinara wa chama cha Economic Freedom Fighters (EFF).

Ingawa sera kuu ya chama chake ni kuwapigania raia weusi ili wajiendeleze kiuchumi, msimamo wake wa kumpenda kila Mwafrika umemnyima umaarufu miongoni mwa wapenda chuki.

Malema naye hajali, wakati wa kampeni za uchaguzi wa awali mwaka huu aliwaambia iwapo ni kosa kuwaambia wawapende Waafrika wenzao, basi wasimpe kura!

Alishikilia kuwa kuwachukia Waafrika wenzao ni sawa na kujichukia wenyewe, akasema hataki kura za watu wanaojichukia kiasi kwamba wanauana na kuwasaza wengineo.

Lakini Malema si mtunga-sera mkuu wa Afrika Kusini, wapo vigogo wanaokohoa tu na kueleweka wanachokinuia hata kabla ya kukisema. Hao chuma chao ki motoni.

Alisema mwanafalsafa Karl Marx kwamba maskini watakapokosa chochote cha kula watawageukia matajiri. Nasema weusi wakitufukuza sote watawaendea viongozi wao.

Wakati huo kila mjasiriamali kutoka mataifa ya Afrika na mengijne yanayoendelea atakuwa ameondoka, Afrika Kusini igeuke kijiji, walane kama majibwa yenye kichaa.

Hiyo itakuwa tiba mwafaka ya uendawazimu unaoendelezwa dhidi ya wahamiaji kutoka Nigeria, Somalia, Kenya, Ghana, Zimbabwe, Pakistan na kwingineko.

Kosa la raia wa mataifa hayo ni kufanya biashara ilhali wanabuni nafasi za kazi na kuwaajiri raia wa nchi hiyo, lakini nafasi yao haitambuliwi.

Mfano wa Jaguar

Wabaguzi na akili zao duni watazuka na kusema hata sisi Wakenya hatutaki wageni wanyemelee biashara tunazoweza kufanya, wakupe na mfano wa Mbunge wa Starehe, Bw Charles Njagua, aliyesema wageni warudi kwao.

Tuliomsuta mbunge huyo limbukeni tulikusudia kuzuia matukio kama yanayoendelea Afrika Kusini. Mwekezaji anapaswa kusaidiwa kuinua biashara yake, si kushambuliwa.

Watu wana maarifa na vipawa tofauti. Si kila mwanadamu aliyejaaliwa uwezo wa kuwekeza na kukuza biashara, aliye na vipawa hivyo anapaswa kulindwa kikamilifu.

Jamii ya kimataifa inapaswa kuingilia kati na kukomesha unyama unaoendelea Afrika Kusini, lau sivyo nayo iingie hatiani ya ubaguzi wa rangi kwa kuruhusu mauaji kuendelea.

 

[email protected]