Habari MsetoSiasa

Mutua akejeliwa kujaribu kuzima ndoto ya Ruto 2022

April 10th, 2018 2 min read

GUCHU NDUNG’U na JOSEPH WANGUI

GAVANA Alfred Mutua wa Kaunti ya Machakos, ameanza rasmi kampeni za kuwania urais mnamo 2022 katika Kaunti ya Nyeri, hali ambayo imekosolewa vikali na viongozi wa kaunti hiyo.

Gavana huyo pia alimfanyia kampeni mwaniaji mmoja wa udiwani, anayegombea kwa tiketi ya chama chake cha Maendeleo Chap Chap.

Hilo limepelekea ghadhabu kutoka kwa wabunge na gavana wa kaunti hiyo, Bw Mutahi Kahiga.

Dkt Mutua alimfanyia kampeni Bw James Ndegwa, anayewania udiwani katika wadi ya Ruguru katika eneobunge la Mathira kwa chama chake cha Maendeleo Chap Chap.

Hii ni licha ya Chama cha Jubilee (JP) kuwa na mgombea katika kinyang’anyiro hicho. Uchaguzi huo mdogo umepangiwa kufanywa mnamo Aprili 18. Hilo ni kufuatia kifo cha aliyekuwa diwani wake, Peter Weru.

Wakiongozwa na mbunge wa Mathira, Bw Rigathi Gachagua, wabunge hao sasa wanamlaumu Bw Mutua kwa kujaribu kuhujumu nia ya Naibu Rais William Ruto kuwanua urais mnamo 2022.

Aidha, walidai kwamba gavana huyo anatumia fedha zilizotengewa kaunti ya Machakos kufanya kampeni hizo.

“Kaunti ya Nyeri haipaswi kutumiwa kama ngome ya kuvuruga mpango wa kisiasa wa Jubilee. Tayari, tuna mwaniaji wetu, ambaye ni Bw Ruto,” akasema Bw Gachagua.

Dkt Mutua aliwasili katika kaunti hiyo mnamo Jumatano wiki iliyopita kwa ziara rasmi ya kikazi ambapo alikaribishwa kwa gwaride la heshima na Gavana Kahiga.

Kwa siku mbili za kwanza, Dkt Mutua alizuru shamba moja la kukuzia maembe, kiwanda cha kutengenezea maziwa, ambapo baadaye alihudhuria hafla ya uzinduzi wa kanuni za utendakazi kwa wafanyakazi wa kaunti hiyo.

Lakini mnamo wikendi, alitembea kutoka kijiji kimoja hadi kingine akimfanyia kampeni Bw Ndegwa. Baadaye alikutana na viongozi wa chama chake katika ukanda wa Mlima Kenya katika hoteli moja karibu na Ikulu Ndogo ya Nyeri.

Gavana huyo pia alifanya mikutano miwili katika eneobunge la Nyeri Mjini. Kwenye mikutano hiyo, alisema kuwa tayari amebuni kundi la kumfanyia kampeni na fedha za kuiendesha atakapowania urais.

“Ninatoa nafasi ya uongozi mwema na wenye uwazi,” akasema.
Hata hivyo, Gavana Kahiga alijitenga vikali na matamshi ya Dkt Mutua, akisema kuwa ukanda wa Mlima Kenya utamuunga mkono Bw Ruto.