Mutua akubali Ruto ni maarufu Mlima Kenya

Mutua akubali Ruto ni maarufu Mlima Kenya

Na SAMMY WAWERU

GAVANA wa Machakos Dkt Alfred Mutua amewataka wakosoaji wa Naibu Rais William Ruto kujua amepenyeza mizizi eneo la Mlima Kenya kwa kiwango kikubwa na umaarufu wake unazidi kupanda.

Dkt Mutua alisema Alhamisi umaarufu wa Dkt Ruto eneo hilo huwezi ukalinganishwa na wa Rais Uhuru Kenyatta, licha ya kuwa ni ngome ya kiongozi wa nchi kisiasa.

Gavana huyo alisema Naibu wa Rais amefanikiwa kushawishi wakazi wa eneo hilo la Kati mwa Kenya kupitia sera zake, akihoji itakuwa vigumu kusambaratisha uhusiano wake na wenyeji.

“Kulingana na utafiti na uchunguzi ambao nimefanya, Naibu wa Rais ndiye anaongoza kwa umaarufu eneo la Mlima Kenya. Ni muhimu tuambiane ukweli.

“Ninamfuata, ila gapu iliyoko kati yangu naye ni kubwa sana. Wakazi wanaamini sera zake, asipuuzwe,” Dkt Mutua akasema.

Gavana huyo alitoa kauli hiyo kwenye mahojiano na runinga ya Citizen, ambapo alikiri ziara za mara kwa mara za Dkt Ruto eneo hilo zimechangia kuwa na umaarufu wa kipekee.

“Awamu ya kwanza ya uongozi wa serikali ya Jubilee, Naibu wa Rais alikuwa akizuru eneo la Kati mwa Kenya na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo. Isitoshe, katika hafla za harambee kama vile ya kanisa na shule, alikuwa akitoa mchango mkubwa na pia kuwasilisha ule wa rais. Ameweza kuwatia mfukoni,” akaelezea.

Matamshi ya Dkt Mutua yanajiri wakati ambapo nyufa kati ya Rais Kenyatta na Dkt Ruto zinaendelea kuwa kubwa na kudhihirisha utengano wao.

Katika awamu ya kwanza ya utawala wa Jubilee, viongozi hao waliitana “mandugu”, Rais akiahidi naibu wake kuwa atakapokamilisha kipindi chake cha miaka 10 atarejesha mkono, kwa kumuunga amrithi kuingia ikulu 2022.

Hata hivyo, ahadi hiyo imeonekana kuwa hewa, hasa baada ya Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga kutangaza kuzika tofauti zao za kisiasa mnamo Machi 2018, kupitia salamu za maridhiano maarufu kama Handisheki.

You can share this post!

Gor Mahia yapigiwa chapuo kuendeleza ubabe kwenye kampeni...

Mwatate, Bomet watoka sare 2-2