Makala

MUTUA: Amerika haijakosea kubagua wahasiriwa wa ugaidi 1998

October 24th, 2020 2 min read

Na DOUGLAS MUTUA

NINASEMA pole na samahani sana kwa Wakenya walioathiriwa na shambulio la bomu lililotekelezwa kwenye ubalozi wa Marekani nchini Kenya miaka 22 iliyopita.

Pole, kwa sababu mpaka sasa hawajapata fidia kamili na huenda wasiipate kwa mujibu wa habari ibuka kwamba Sudan imeamua kufidia Wamarekani pesa nyingi kuliko Wakenya.

Samahani, kwa sababu huenda baadhi ya mambo ninayonuia kuandika hapa hayatawapendeza Wakenya walioathirika.

Juzi Marekani imeishinikiza Sudan mpaka ikakubali kutoa fidia ya jumla ya Sh36 bilioni, lakini kiasi kikubwa kilipewa Wamarekani huku Wakenya wakipata kifutia machozi tu.

Familia ya Mmarekani yeyote aliyeuawa kwenye shambulio hilo la kigaidi atalipwa takriban Sh1 bilioni huku ile ya Mkenya aliyeuawa akifanya kazi ubalozini hapo italipwa Sh87 milioni.

Raia wa Marekani waliojeruhiwa watalipwa Sh326 milioni huku Wakenya waliojeruhiwa na ambao walikuwa wafanyakazi hapo wakilipwa Sh43 milioni.

Nimesisitiza ‘Wakenya waliokuwa wakifanya kazi hapo’ kwa sababu wengine wote waliouawa ama wakiwa kwenye shughuli rasmi ubalozini hapo au wakipita kujiendea zao hawatafidiwa!

Sawa na Wakenya walivyofanyiwa mkasa huo ulipofanyika, na Marekani ikashughulikia raia wake kwa njia bora zaidi, sasa wanailaani Marekani na kudai inawabagua Wakenya.

Sudan pia imo lawamani kwa kukubali kuwafidia Wamarekani vyema zaidi kuliko Wakenya. Wengi wanalalamika kwamba taifa hilo la Afrika linapaswa kuwatendea haki Waafrika.

Wanaolalamika wanahoji kwamba hii ni ithibati eti maisha ya Mwafrika yana thamani ya chini sana yakilinganishwa nay a Mmarekani.

Swali langu ni hili: katika harakati za kuwatafutia fidia majeruhi na manusura wa mkasa huo, anayekadiria thamani ya maisha ni nani na anafaidikaje akilinganisha Wamarekani na Waafrika?

Kwa taarifa yako, serikali mpya ya Sudan imekubali kutoa mafedha hayo ili Marekani iondoe taifa hilo kwenye orodha ya mataifa yanayofadhili ugaidi.

Kisa na maana ni kuwa aliyekuwa kiongozi wa kundi la Al-Qaeda, Osama bin Laden, alijificha nchini Sudan akipanga shambulio hilo.

Mtazamo kuwa serikali za Sudan na Marekani zinawabagua Wakenya unaweza tu kushikiliwa na mtu ambaye hataki kutafakari na kuchanganua mambo na kupata uhalisia wake.

Kwanza tukubaliane kwamba Serikali ya Marekani ina majukumu ya kuwatetea na kuwalinda Wamarekani pekee, hivyo maslahi ya Wakenya yanapaswa kushughulikiwa na Serikali ya Kenya.

Pili, kikawaida serikali yoyote haitoi fedha, au vinginevyo, hadi pale itakapokabiliwa na nguvu za kuitishia au shinikizo la kuiudhi kiasi cha kutotulia na kutenda kazi kwa amani.

Hii ina maana kwamba Sudan haikupata tishio lolote kutoka kwa serikali ya Kenya; hata ingekataa kuwalipa chochote Wakenya walioathiriwa haingechukuliwa hatua zozote na Rais Uhuru Kenyatta.

Kenya haina orodha yoyote ya mataifa yanayofadhili ugaidi wala haihitaji kuwa nayo kwa sababu haitazidisha wala kuounguza chochote. Kenya ni taifa dhaifu linaloendelea, hivyo mkasa uliotokea miaka 22 si dharura ya kuwakosesha usingizi viongozi wake.

Kimsingi, ninawaambia wanaolalamika kuhusu fidia ndogo kwa Wakenya kwamba aliyeishusha thamani ya maisha si mwingine bali serikali ya Kenya.

Huku Marekani ikiwana usiku na mchana kuwashinikiza viongozi wapya wa Sudan watoe mafedha ya fidia ili taifa lao likubalike tena kwenye jamii ya kimataifa, Kenya haishughuliki!

Kenya, ambayo ilimtambua na kumthamini aliyekuwa kiongozi wa Sudan, Omar al-Bashir aliyepinduliwa miaka miwili iliyopita, haijafanya chochote kuwashinikiza viongozi wapya wa Sudan walipe fidia.

Nimeandika hapa mara kadhaa kwamba serikali ya Kenya haithamini maisha ya Wakenya, wawe nchini au ughaibuni, ndiyo maana tunatendewa vyovyote tu na watu wengine.

Viongozi wa Kenya wanajithamini wenyewe na familia zao pekee, ndiyo maana wamo mbioni kubadili Katiba ili waunde na kugawana vyeo miongoni mwao huku makabwela wakienda miayo.

Ikiwa Mkenya anataka kupandisha thamani ya maisha yake, itabidi aanze kwa kujichagulia viongozi adili na adibu, si wabinafsi na walafi mfano wa fisi ambao wanatuongoza kwa sasa.

[email protected]