MUTUA AMTIA UHURU PRESHA

MUTUA AMTIA UHURU PRESHA

BENSON MATHEKA Na PIUS MAUNDU

Wakenya wamemtaka Rais Uhuru Kenyatta kuiga mfano wa Gavana wa Machakos Alfred Mutua kwa kuwapatia afueni ya ushuru kufuatia kanuni kali alizotangaza kukabiliana na wimbi la tatu la janga la corona.

Rais Kenyatta hakutangaza hatua zozote za kukinga wakazi milioni 12 wa kaunti za Machakos, Nairobi, Kiambu, Kajiado na Nakuru alizofunga kwa muda usiojulikana.

Jana, Gavana Mutua alitangaza hatua kadhaa za kuwakinga wakazi wa kaunti ya Machakos dhidi ya hali ngumu ya maisha inayosababishwa na kanuni za kuzuia msambao wa virusi hivyo.

Hatua hizo zinalenga wakazi wa mapato ya chini wakiwemo wahudumu wa matatu, mama mboga, wauzaji wa matunda, waendeshaji wa bodaboda, wahudumu wa matatu na wamiliki wa biashara ndogo ndogo.

Dkt Mutua alisema viongozi wa kisiasa wanafaa kuwa katika msitari wa mbele kutoa suluhu kwa matatizo ya Wakenya wakati huu wanapokabiliwa na hali ngumu ya maisha badala ya kushughulika na siasa za uchaguzi mkuu wa 2022.

“Wanasiasa hawafai kuongozwa na ulafi, na kupanga siasa za 2022. Wanafaa kuonyesha moyo wa utu na kuweka hatua za kuinua maisha ya watu wetu ambao wanakabiliwa na wakati mgumu wakati huu wa janga la corona,” Bw Mutua alisema.

Katika hatua iliyoonekana kumshinikiza Rais Kenyatta kutoa afueni kwa Wakenya wakati huu wa kanuni kali za kukabili wimbi la tatu la corona, Dkt Mutua alimuomba kiongozi wa nchi aagize kampuni ya stima isiwakatie stima watakaoshindwa kulipa bili.

“Ilivyokuwa awali, ninaomba Rais aingilie kati ili kampuni ya Kenya Power isikatie stima Wakenya wanaokabiliwa na wakati mgumu wakishindwa kulipa bili,” alisema Dkt Mutua.

Pia, aliitaka Mamlaka ya Kudhibiti sekta ya Kawi (EPRA) kupunguza bei za petroli na mafuta taa zinazoumiza Wakenya.

Kiongozi huyo wa chama cha Maendeleo Chap Chap, alifuta ada zote zinazotozwa wahudumu wa bodoboda kila siku kaunti ya Machakos, akasitisha ada zote za wahudumu wa tuktuk hadi Juni 30 na pia akafuta riba kwa waliochelewa kulipa ada za ardhi kwa muda wa siku 45.

Ili kukinga wahudumu na wamiliki wa matatu ambao wameathiriwa pakubwa na marufuku aliyotangaza Rais Kenyatta, Dkt Mutua alipunguza ada za kusajili wahudumu wa magari ya uchukuzi wa umma kwa asilimia 50.

“Mama mboga hawatatozwa ada zozote,” aliagiza gavana huyo.

Alihimiza wamiliki wa nyumba za kukodisha kutowafukuza wanaoshindwa kulipa kodi.

“Wakenya wengi wanang’ang’ana kulipa kodi ya nyumba. Ninaomba landilodi kupunguza kodi za nyumba kwa muda fulani. Pia, ninawaomba kuwa wavumilivu wakati mpangaji anapochelewa kulipa kodi wakati huu mgumu,” alisema Dkt Mutua.

Katika hatua ya kukinga biashara ziziporomoke, Dkt Mutua alipunguza ada za leseni za biashara kwa asilimia 50. Alipatia afueni sawa kwa shule zote za kibinafsi na taasisi za elimu katika kaunti hiyo.

“Hii ni nchi yetu na kama viongozi, tunafaa kutoa suluhu kwa matatizo yaliyo katika mikono yetu na raia wetu. Ndani yetu, tuko na nguvu za kusaidiana kuinua maisha ya kila mmoja. Tuwe na mioyo ya kujali. Tunapofanya hivi, sote tutainuka na kuishi maisha yaliyobarikiwa,” alisema.

Wakazi wa kaunti hiyo walifurahishwa na hatua ya gavana wao huku wale wa kaunti nyingine wakimuomba Rais kufuata nyayo zake.

Wahudumu wa sekta ya utalii wamelalamika kuwa marufuku ya serikali itaporomosha sekta hiyo.

Peter Nzomo, anayechuuza matunda katika soko la Kithimani kwenye barabara kuu la Thika Garissa alisema walikuwa wanapata hasara kwa kuwa magari kutoka kaunti nyingine hayaruhusiwi kuingia kaunti ya Machakos.

You can share this post!

Maradhi Ya Kutatizwa Na Figo yaongezeka nchini

China yaanza kutoa chanjo ya Covid-19 kwa wageni wa mataifa...