MUTUA: Chocheo la vita Ethiopia ni ukabila, manyanyaso

MUTUA: Chocheo la vita Ethiopia ni ukabila, manyanyaso

Na DOUGLAS MUTUA

VITA vinavyoendelea nchini Ethiopia ni mfano bora wa mambo yanavyoweza kuharibika mfumo wa utawala wa ugatuzi usipotekelezwa vizuri.

Nchini humo, kila eneo linajitawala kiasi cha kuwa na vikosi vya usalama visivyo chini ya usimamizi wa polisi na majeshi ya kitaifa.

Mbali na vikosi halali vya majimbo, takriban kila eneo na kabila lina waasi wanaofanya mazoezi kila siku kuipindua serikali ya kitaifa! Ugatuzi wa vyombo vya usalama umegeuka tishio dhidi ya usalama wenyewe.

Ukabila nao umekita mizizi kwa muda mrefu; kabila la waziri mkuu huchukuliwa kama linalopendelewa kwa mafedha na mamlaka serikalini.

Hisia za mapendeleo zinazidishwa na hatua ya serikali ya Ethiopia kukataa kuyagawia majimbo fedha za kutosha kama inavyotakiwa kikatiba.

Katika nchi hiyo ya watu zaidi ya milioni 100, makabila ambayo yanajihisi kutengwa na serikali yao hutafuta mbinu za ama kujikimu au kuling’oa gugu sugu linalojiotea litakavyo.

Vita vinavyoendelea baina ya serikali na waasi wa Tigray People Liberation Front (TPLF) ni matokeo ya utekelezwaji maovu wa ugatuzi.

La kushangaza ni kwamba kundi la TPLF limejifunga vibwebwe kupambana na serikali ili kupinga maovu ambayo lenyewe lilitenda kwa miongo zaidi ya miwili.

Aliyekuwa kiongozi wa TPLF, marehemu Meles Zenawi, aliongoza nchi hiyo kama waziri mkuu alipopindua serikali ya Mengistu Haile mariam mnamo 1991.

Kundi hilo lilifaidi raha zote za madaraka bila bughudha hadi Meles alipofariki mnamo 2012.

Wakati wa uhai wake, Meles alihakikisha takriban asilimia 50 ya vyeo vya juu katika jeshi na serikali vilishikiliwa na watu wa kabila lake dogo sana la Tigray.

Wahabeshi kwenye nchi za watu walilalamika kwamba Wa-Tigray waliochoka kuishi ughaibuni wakirejea tu wakisaidiwa kuanzisha biashara au kupata ajira nzuri serikalini.

Watu wa makabila mengine hawangethubutu kurejea kwa kuwa waliofanya hivyo wakishukiwa na kufuatwa unyo-unyo na majasusi kokote walikokwenda. Baadhi yao wakikamatwa na kusingiziwa kuwa majasusi wa kigeni.

Waliojificha nchini Kenya wakiandamwa, kukamatwa na kurejeshwa Ethiopia ambako walipelekwa gerezani moja kwa moja.

Meles alipofariki alirithiwa na naibu wake, Dkt Hailemariam Desalegn, na ghafla minung’uno ikaanza iwapo wahafidhina wa Tigray wangemruhusu kutawala.

Wahabeshi walitania ati Desalegn alikuwa waziri mkuu kinyago tu kwa kuwa walioiongoza Ethiopia hasa ni maafisa wanne wa ngazi za juu, wote wa kabila la Tigray!

Makabila makubwa yalipochoka kukaliwa mguu wa kausha na Tigray yalikula njama kumshinikiza Dkt Desalegn ajiuzulu, bungeni yakamchagua Dkt Abyi Ahmed Waziri Mkuu.

Alikuwa na lazima ya kuibomoabomoa na kuifagilia mbali miundo-mbinu iliyowapendelea na kuwadekeza Watigray iwapo angetaka kutawala kwa njia salama.

TPLF, ambayo awali iliongoza muungano wa vyama kadha uliounda serikali, ilisombwa mbali na ikajua si kwema, ikarejea zizini kama ng’ombe aliyevunjikia mguu malishoni.

Maafisa wa TPLF waliokuwa katika ngazi ya kitaifa walijiunga na serikali ya jimbo la Tigray na ghafla wakakosana Dkt Ahmed walipokaidi amri yake kwamba wasiandae uchaguzi mwaka jana.

Mnamo Novemba mwaka jana, Dkt Ahmed aliwatuma wanajeshi hadi Tigray, wakaua watu na kuipindua serikali ya jimbo kisha akawateua watawala wapya.

Si hayo tu! Alipiga marufuku TPLF na kuitangaza kundi la kigaidi! Huko nyikani vita viliyalemea majeshi yake, yakatekwa kwa maelfu na waasi wa TPLF! Alisitisha mapigano ghafla.

Alishindwa vita kwa kuwa maafisa wa kabila la Tigray walioshikilia asilimia zaidi ya 40 ya vyeo vya jeshi la kitaifa wakati wa utawala wa Meles walishajiunga na TPLF.

Sasa kamanda mkuu wa TPLF, Jenerali Tsadkan Gebretensae, ameapa kuingia Addis Ababa kwa mshindo ili kuipindua serikali ya Dkt Abyi Ahmed!

Anga itanuka baruti! Na maelfu – labda mamilioni – ya watu wasio na hatia watakufa kwa vita na kiangazi kinachotishia kuigubika Ethiopia.

Jamii ya kimataifa ina jukumu la kumaliza mzozo huo lau sivyo wakimbizi waanze kumiminika kote Afrika Mashariki na Kati.

mutua_muema@yahoo.com

You can share this post!

Pochettino matumaini juu PSG ikigaragazana na Lille katika...

KAMAU: Ufanisi wa nchi unategemea viongozi tunaowachagua