Makala

MUTUA: Corona haiathiri Wazungu tu wengi wanavyofikiria

April 5th, 2020 2 min read

Na DOUGLAS MUTUA

KATI ya mambo ya kipumbavu niliyowahi kusikia kuhusu ugonjwa wa virusi vya corona ni kwamba, ni ugonjwa wa matajiri na si wa Mwafrika.

Dai hilo linaloibua hisia za kibaguzi kwa misingi ya rangi lilififia ghafla ugonjwa wenyewe ulipotua barani na kuanza kusambaa kwa kasi. Inasemekana mambo bado!

Uliporipotiwa kuenea kwingi duniani mapema mwezi jana, watu wengi walitumia mitandao ya kijamii kuupuuzilia mbali na kuonyesha kuwa si tishio kwa maisha ya watu wa kawaida.

Walioonyesha mapuuza hayo walitoa mifano ya maradhi mengine duniani kama saratani, kifua kikuu, malaria na homa kali ambayo yanaua watu wengi zaidi.

Ukweli wa mambo ni kwamba, virusi vya corona havichagui, havibagui. Vinaenea kokote, kwa maskini na matajiri, sikwambii vinaua hivyohivyo.

Waliodai ni ugonjwa wa matajiri walisema hivyo kwa sababu huu ni ugonjwa wa kwanza ambao umeambukiza na kuua watu wengi mashuhuri katika muda mfupi mno.

Labda dhana hiyo potovu ilitokana na ukweli kwamba, ugonjwa wenyewe ulianzia Uchina na kusambaa kwingineko, bila shaka kupitia usafiri wa watu kwa ndege au hata meli.Unachopaswa kujua ni kwamba, kuabiri ndege au meli si kuwa tajiri.

Wapo watu ambao husafiri ikibidi, yaani wangekuwa na chaguo hawangesafiri, hivyo kumchukulia aliyeingia ndani ya ndege kuwa tajiri ni ushamba wa kupigiwa mfano.

Ninapokuandikia hivi, mtangazaji maarufu wa shirika la CNN, Chris Cuomo, anatangazia kwenye chumba cha chini alikojifungia mbali na mkewe na watoto baada ya kuambukizwa.

Watu wengine maarufu walioambukizwa ni pamoja na Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson, mshauri wake mkuu wa masuala ya afya pamoja na waziri wake wa afya.

Vilevile, mwana wa kifalme wa Uingereza Prince Charles na mke wa Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau, Bi Sophie Grégoire Trudeau, wameambukizwa na kujifungia.

Natumaini hujasahau kwamba meneja wa klabu ya kabumbu ya Arsenal, Mikel Arteta, alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza mashuhuri kugunduliwa kuwa na ugonjwa huo.

Madaktari wakuu wenye tajiriba nyingi, viongozi na watu wengine mashuhuri duniani wameuawa na coronavirus.

Yapo makumi, ikiwa si mamia, ya watu mashuhuri ulimwenguni waliofariki baada ya kupata ugonjwa huo, lakini nakutolea mifano ya Afrika tu, karibu na nyumbani.

Tulipoteza pakubwa pale wanamuziki wawili maarufu barani, ambao watakumbukwa milele kwani wamo kwenye kumbukumbu za historia, walipofariki.

Daima tutawakumbuka Emmanuel N’Djoké “Manu” Dibango, raia wa Cameroon aliyesifika kwa muziki chapa Jazz, na Aurlus Mabele, Mkongomani anayesifika kama ‘Mfalme wa Soukous’. Mifano niliyokutolea imejulikana kutokana na umaarufu, lakini ukweli ni kwamba watu wa kawaida wanaendelea kufariki kutokana na ugonjwa huo.

Na jambo la kuhuzunisha zaidi ni kwamba, ungali kitendawili kigumu kuteguliwa na wanasayansi wakuu duniani, wote wanajaribisha tiba hii na ile, ukipona ‘ahsante Mungu’.

[email protected]