Makala

MUTUA: Corona si mzaha, jizuie bila kuitegemea serikali

November 21st, 2020 2 min read

Na DOUGLAS MUTUA

WINGU jeusi linatanda juu ya anga ya Kenya, kisa na maana janga la korona.

Mombasa maeneo ya makaburi yanajaa upesi kuliko kawaida kwa kuwa vifo vya korona vimezidi.

Kote nchini, walimu wakuu zaidi ya 13 wa shule za upili wamefariki kutokana na ugonjwa huo.

Wanasiasa kadhaa, hasa wawakilishi wa wodi wametuaga na inakisiwa kuwa wengine wengi wanaugua.

Watu mashuhuri kama mawakili na maprofesa pia wamefariki kutokana na ugonjwa huo.

Hayo ni makundi machache ya watu wenye hadhi katika jamii, ambao ni rahisi kuripotiwa lolote baya likiwatokea.

Je, mwananchi wa kawaida ambaye akifariki hata utafiti haufanywi kujua kilichosababisha kifo au hali yake ikoje inatabirika?

Ajabu akidi ni kwamba bado kuna watu wasioamini kwamba ugonjwa huo upo au unaua kwa wingi nchini Kenya.

Wapo wanaoshikilia ule msimamo wa kishamba kwamba korona ni ugonjwa wa ughaibuni, eti unamaliza wazungu na watu wengine ambao si weusi.

Hao ukiwaambia hata ughaibuni, hasa Marekani, watu weusi wanaugua corona na kujifia ovyo, ni wepesi wa kujibu kwamba huu ni ugonjwa wa matajiri. Utadhani ufukara una chochote cha kuringia!

Jamani! Wakati umepita wa kulifanyia mzaha janga hili la korona. Huu si wakati wa kutaniana kuhusu nani kajaaliwa au kapungukiwa na nguvu za kumkinga na maradhi.

Nakumbuka nikiandika papa-hapa kwamba hatua ya kulegeza masharti ya kukabiliana na corona iliyochukuliwa na Serikali isichukuliwe visivyo kwamba hatari imetoweka.

Wakati huo niliudhika hadi ya kuudhika nilipoona watu wakifunga safari kuzuru mashambani kutoka mijini kana kwamba Serikali kawapa sikukuu ndefu.

Mambo kama hayo ya kuchukua hatua bila kutafakari matokeo huashiria mtu hawajibikii maisha yake mwenyewe, anaitegemea serikali kufanya hivyo.

Iwapo hujapima ukajua una corona au la, na unakwenda mashambani kuwaona wazee wako, basi jua unahatarisha maisha yao kwa kutotumia akili sawasawa.

Serikali haitakuandikia barua kukukumbusha eti wazee wako wamo katika hatari kubwa zaidi ya kuambukizwa na hata kufariki. La hasha! Itakuacha utumie akili na ukishindwa ukubali matokeo ya uzuzu wako.

Kenya ni nchi ambamo mtu anapaswa kuwa mwangalifu kabisa na kuhakikisha anawajibikia kila hatua anayopiga.

Ninasema hivi kwa sababu serikali yenyewe haitekelezi wajibu wake ipasavyo, hivyo ukijiachia ovyo unakabiliwa na hatari mbili: kujitelekeza mwenyewe na kutelekezwa na serikali.

Hebu tazama: huku mataifa mengine duniani yakiwa mbioni kuagiza chanjo ya corona kwa mapema hata kabla haijakamilika kutengenezwa, wanasiasa wa Kenya wanafikiria kuhusu atakayekuwa rais ifikapo 2022.

Wanasiasa wanacheza kamari haramu na maisha yako kwa sababu kati ya sasa na uchaguzi mkuu ujao hakuna jingine muhimu kuzidi uchaguzi.

Hata hiyo kura ya maamuzi ya BBI inayopigiwa upatu sana na wakuu wa serikali na upinzani rasmi isikupumbaze; ni mbinu yao kujitafutia msisimko wa kati ya sasa na wakati huo.

Hawajali wapigakura wengi wakiuawa na korona atakayewachagua ni nani kwa sababu kwa vyovyote vile, hata ikiwa ni watu 200 pekee watakaopiga kura, atakayechaguliwa ndiye atakayeiongoza Kenya kwa miaka mitano.

Si siri kwamba wanasiasa wangependa sana kushughulikia kikundi kidogo cha wapigakura badala ya mamilioni. Umati una gharama eti, hali mamlaka anayopata anayechaguliwa na wachache au wengi ni yaleyale. Mbona mwanasiasa agharamike?

Hali ikiwa hiyo unajua unaishi ndani ya chaka kuu na humo ndani mna simba, chui, duma, tembo, nyati, vifaru na wanyama wengine wakali.

Kwa hivyo? Jukumu la kuwa salama au la linakuwa wajibu wako.

Usitarajie serikali ikuletee chanjo wala tiba kutoka ughaibuni. Ikibidi watajiletea viongozi wakuu na kujiwekea kama akiba ili hatari ikiwatokea na watoto wao watibiwe na kusalia hai. Wanasema hata wakikuletea tiba huwezi kuzimudu gharama za matibabu.

Hivi, ikiwa una akili japo za wastani, utakosaje kujihadhari na kuwaweka salama jamaa zako ukiishi nchi kama hiyo, Kenya katika muktadha huu?

Huu si mzaha tena, corona inaangamiza kikweli. Ikiwa unapenda kuishi hai, jihadhari mwenyewe.