Makala

MUTUA: Kuna matunda tele Afrika Mashariki kushikamana

September 21st, 2019 2 min read

Na DOUGLAS MUTUA

JUHUDI za kuleta amani kati ya Uganda na Rwanda zilizoanzishwa na taifa la Angola zimenipa mtihani wa kufikiria kama Mkenya na Mwafrika kwa jumla.

Niliwaza kwa kuzingatia kwamba Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya ndiye aliyejaribu kuwapatanisha Rais Yoweri Museveni wa Uganda na Rais Paul Kagame wa Rwanda mapema mwaka huu.

Wakati huo, nilishangaa Rais Kenyatta alikuwa na tajiriba gani ya kuwapatanisha watu wawili walioingia madarakani kwa mtutu wa risasi ilhali mwenyewe alichaguliwa.

Wakati huu, kwa kuamini hatua ya Rwanda kuanzisha mazoezi ya kijeshi kana kwamba kujiandaa kukabiliana na Uganda ilizaa matunda, ninaiwaza nchi yangu.

Akazuka kichaa jirani, mfano Museveni, aagize majeshi yake yaanze kufanya kazoezi ya kijeshi kwa madhumuni ya kutushambulia tungefanyaje?

Si kwamba Majeshi ya Ulinzi ya Kenya (KDF) hayana uwezo wa kututetea vikali dhidi ya mashambulizi kutoka nje, lakini sijui utawala wetu wa kiraia umejiandaliaje hali kama hiyo.

Ilitabirika rahisi kwamba, Rais Kenyatta angenoa pakubwa katika juhudi zake hizo kwa maana fikra zake na za viongozi hao wawili ziko mbalimbali kama mbingu na ardhi.Rais Museveni na Rais Kagame walikutana msituni walipokuwa waasi, zama hizo wakipigana na serikali ya Uganda.

Waliposhinda vita na kutwaa madaraka, Museveni aliutwaa urais na kumpa Kagame, raia wa Rwanda, cheo cha jasusi mkuu wa kijeshi.

Baadaye, Museveni alimsaidia Kagame na waasi wake kuing’oa mamlakani serikali ya kihutu iliyowakandamiza raia wa jamii ya Watutsi na hata Wahutu wa msimamo wa kadri.

Ni sahihi kusema kwamba, fikra za Museveni na Kagame ni sawa, wanaheshimiana kwa namna fulani kwa kuwa kila mmoja anafahamu uwezo wa mwenzake.

Lakini huwezi kusema hivyo kumhusu Rais Kenyatta, mwana wa kifalme aliyelelewa ikulu na mazingira ya kikasri, asiyewahi kulala nje akipigania chochote wala yeyote.

Nina hakika machoni pa Museveni na Kagame, Rais Kenyatta ni mcheshi asiyeyafahamu masuala ya ukombozi hata kidogo. Si ajabu hawakumsikiza.

Haishangazi juhudi za sasa za kuwapatanisha wawili hao zinaongozwa na Rais Joao Lourenco wa Angola, mwanajeshi mstaafu aliyeshiriki vita vya kumfukuza mkoloni.

Ungewasikia hivi majuzi wajumbe wa amani wa pande zote mbili wakiapiana kuutekeleza kikamilifu mkataba wa amani uliotiwa saini na viongozi wao ungejiuliza walikosanaje.

Rwanda na Uganda zina uhusiano wa karibu mno kuanzia kwenye utamaduni, siasa, na biashara, sikwambii Rais Museveni mwenyewe anakisiwa kuwa na asili ya Rwanda.Kutokana na uhusiano huo wa miaka mingi, uhasama kati ya nchi hizo uliosababisha raia na bidhaa zao wazuiwe kutembeleana haikosi umewaathiri vibaya wadau.

Nchi zenyewe zimeathirika kiuchumi, familia zimetenganishwa, navyo vikosi vya usalama vimewekwa kwenye hali ya tahadhari visipepese macho kwa hofu ya kushamuliwa.

Hakuna watu wanaopaswa kuishi hivyo katika Karne hii ya 21 eti kwa sababu viongozi wao wangali wanaota wakihujumiana na kung’oana madarakani.

 

[email protected]