Makala

MUTUA: Morsi hakuwa dikteta na kifo chake ni huzuni

June 21st, 2019 2 min read

Na DOUGLAS MUTUA

KIFO cha aliyekuwa Rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini Misri, Dkt Mohamed Morsi, lazima kimewasononesha viongozi wengi duniani.

Labda ungetarajia niseme kimewasononesha madikteta wengi duniani, lakini nakataa kusema hivyo kwa maana Dkt Morsi hakuwa dikteta.

Tofauti za kiitikadi kati ya serikali yake na raia waliozoea utawala usio na udini kama wa kundi lake la Muslim Brotherhood zililipa jeshi fursa ya kutwaa mamlaka.

Hii ina maana kwamba si lazima uwe kiongozi dhalimu ili upinduliwe; raia wakimwagika barabarani na kukulaumu kwa chochote kile, majeshi yanaweza kuamua kuingilia kati.

Tatizo la huko kuingilia kati ni kwamba jeshi likiipindua serikali halina haraka ya kuondoka madarakani, linaweza kutawala milele.

Ndivyo mambo yalivyo nchini Misri wakati huu. Jenerali Abdel Fattah al-Sisi, aliyekuwa mkuu wa majeshi na waziri wa ulinzi wa serikali ya Dkt Morsi, alijiuzulu jeshini akawania urais na hana haraka ya kuondoka.

Waulize raia wa Sudan walioandamana dhidi ya Rais Omar al-Bashir miezi kadhaa iliyopita mambo yalikwenda vipi.

Walidai wamejikomboa, kufumba na kufumbua jeshi likatwaa mamlaka yote na kuanza kuwauliza wangetaka wagawiwe vyeo gani! Wangali wanajadiliana.

Kifo cha Rais Morsi ni ithibati kwa viongozi waliotarajia labda angerejea madarakani kwamba uking’olewa ndio basi, kila kitu kinakuporomokea mpaka mwisho.

Bila shaka walio na hofu zaidi ni viongozi wa mataifa ya kiarabu, hasa wanaozitawala nchi zao kimabavu, zinazojitia hamnazo kuhusu nguvu za mataifa ya magharibi.

Hao nakwambia wamepata taswira kamili ya uwezekano wao kufia jela baada ya kupinduliwa. Wamejionea Rais Morsi, ambaye aliwapendelea zaidi wenzake wa kundi la Muslim Brotherhood huku akiwapuuza raia wengine wa Misri.

Walijionea Rais Muammar Gaddafi wa Libya aliyelitenga eneo dogo la Benghazi, maasi yakazuka huko, mataifa yenye nguvu yakaingilia, akapinduliwa na kuuawa kinyama.

Vilevile walijionea Saddam Hussein aliyewanyanyasa Waqurdi mpaka wakakimbilia uhamishoni, msururu wa mambo ukafuata mpaka akapinduliwa.

Haikosi viongozi wa mataifa ya kiarabu wangali wanakumbuka picha ya kuogofya ya Saddam alipofukuliwa kutoka kwenye shimo alimojificha, kaliwa na wadudu wa kila aina!

Picha ya mwisho ya Saddam ni alipovishwa kitanzi, hatima yake ikawa ndiyo hiyo, akaondoka duniani katika muda wa sekunde chache tu.

Anayepitiwa akilini na taswira hiyo zaidi ni Omar al-Bashir, ambaye sasa ni mahabusu, sikwambii amefunguliwa mashtaka yanayoweza kumweka jela milele au anyongwe!

Nimeamua kulenga mataifa ya Kiarabu kwa sababu kwa namna fulani yamekataa kufungamana pakubwa na mengineyo duniani.

Waulize raia wa mataifa ya Kiarabu watakwambia wao ni watu huru, si watumwa wa Marekani, Ujerumani, Urusi wala Uingereza.

Sijui manufaa ya kujitenga huko, lakini athari zake hasi nazijua vizuri: Ikifika siku ya kukandamizwa kabisa na mahayawani wanaoita watawala wao, msaada hufika kuchelewa.

Thubutu!

Thubutu kupindua serikali ya taifa lolote Afrika bila kukubaliana na mataifa hayo ya Magharibi, utazimwa alfajiri na majeshi yao yaliyo kotekote!

Hilo hutupa uthabiti fulani.

Hata hivyo, viongozi wetu pia huishi na hofu kwamba huenda baadhi yetu wakaungwa mkono kutoka ugenini na kuwatimua kutoka madarakani, hivyo hawaishi kutafuta urafiki na mataifa hayo.

Si vibaya, lakini nadhani muhimu zaidi ni viongozi kuwa wazalendo wa kweli – wanaoongoza kwa haki na ukweli – bila mapendeleo yoyote.

Ushauri wangu kwa viongozi: usiwape raia sababu za kuandamana na kukushinikiza ujiuzulu; watawapa wanajeshi kisingizio cha kutwaa mamlaka.

Na yakitwaliwa hali ya kiongozi na raia ni moja: huku kiongozi akifungiwa korokoroni na kufia huko, raia watavunjiwa haki na kufanywa maskini mpaka wakati wasiojua.

Hali ikiwa hiyo, ndoto ya raia kujikomboa haifikiki, nchi huzorota kila nyanja, haki za binadamu zikavunjwa kiholela, kutamauka kukawa ndio mtindo wa maisha.

[email protected]