Makala

MUTUA: Mwafrika anajihini mengi kuchukia nduguye mweusi

April 4th, 2019 2 min read

Na DOUGLAS MUTUA

HIVI chuki hii ya Mwafrika dhidi ya Mwafrika mwenzake anayeamua kuhamia ughaibuni kujitafutia riziki ilitokana na nini?

Juzi nilisoma mzaha fulani kwenye mtandao ukanipa changamoto kutafakari kuwahusu Wakenya na Waafrika kwa jumla.

Mzaha wenyewe ulisema kwamba wivu ndiyo hatua ya mwisho katika mchakato wa kuwa mchawi. Bila shaka huo ni mtazamo wa mtu mbunifu tu, si aya ya Qur’an wala Biblia.

Hata hivyo, ikiwa huoni ugumu kuyatumia mambo ya kawaida kuweka maisha kwenye mizani, utatambua kwamba aliyetunga mzaha huo alikuwa katika roho na kweli.

Sheria zinapotungiwa kundi la watu, eti wakichukua uraia mwingine kisha wanyamaze watafungwa jela miaka mitatu au watozwe Sh5 milioni, ukiwa mkweli utatambua wivu.

Unaweza kukana ukweli huu na kusema labda ni chuki ya kibinadamu tu, lakini nitakwambia msukumo wa chuki hiyo si kitu kingine ila wivu.

Ni wivu unaotokana na dhana kwamba mtu akiabiri ndege ‘ametoboa’ kimaisha, ukihisi huna jinsi ya kufikia alikofikia ukaamua kumtafutia visingizio vya kumkata miguu.

Ikiwa Katiba ya Kenya imesema wazi hakuna anayeweza kukupokonya uraia wako ukiwa mzawa, kujaribisha vikwazo vya hapa na pale ni kudhihirisha udhaifu wa asasi husika.

Ingawa watu wanaohamia nchi za watu hutuma mabilioni ya pesa nchini Kenya kusaidia familia zao na wala si kwa serikali moja kwa moja, pesa hizo za kigeni hukuza uchumi.

Dola au pauni za Wakenya walio ughaibuni hufanikisha makuzi ya uchumi kwa manufaa ya waliobaki nchini na hivyo basi haki zao hazipaswi kuchukuliwa kama hisani kutoka kwa serikali.

Unaweza kupuuzilia mbali mchango wa jumla wa hao wanaoishi ughaibuni, useme hujawahi kupokea msaada wa moja kwa moja kutoka kwao, lakini labda ni sasa tu.

Huenda siku za usoni Afrika nzima ikategemea hisani ya hao wanaoishi nchi za watu kuijenga upya ikibomolewa kabisa na Wachina au majanga ya kiasili.

Juzi niliposikia habari kwamba mjamzito alilazimika kujifungua huku kaning’inia mtini akihofia kusombwa na tufani ya Idai nchini Mozambique niliwaza mengi.

Nilikumbuka kwamba tangu tukiwa watoto mpaka sasa tumesadikishwa kwamba Afrika haina mgao wowote wa vimbunga na majanga mengine ya kiasili sampuli hiyo.

Lakini sasa yametua barani kwetu na kutupata tukila chakula kibichi, tukiishi nyumba za kukandikwa udongo, taa ni ya tandika-nilale, nishati ni kuni ngumu na kadhalika!

Hii ina maana kwamba mabadiliko ya tabianchi yatakuwa na athari mbaya mno barani kwetu kwa maana miundomsingi ama haipo au ni duni kupindukia.

Msimu wa baridi kali kama unaoshuhudiwa Ulaya ukitokea Afrika, karibu watu wote wasio na nguvu za umeme wataangamizwa na baridi na maradhi!

Kimbunga kikuu kikitokea na kuyaangusha majumba makubwamakubwa unayoyaona mijini, wengi wataangamia kwa sababu ya ukosefu wa vifaa na huduma duni za uokoaji.

Watu wachache watakaosazwa na majanga ya aina hiyo watakuwa na kibarua kigumu kulijenga bara zima upya kivyao kwa sababu hawatakuwa na uwezo wa kufanya hivyo.

Hapo ndipo hao wahamiaji wa nchi za watu wanaochukiwa na wenyeji wa sasa wa Afrika watakaporejea kujenga upya bara lao.

Hapo ndipo Wamarekani Weusi na watu wengine wote ambao ni vizazi vya wenzetu waliouzwa utumwani na Waafrika wa zamani watakaporejea na kudai kulikokuwa kwao.

Ukitaka sema haya ni maoni ya kufikirika tu, lakini kumbuka uhalisia ni zao la fikira. Haikukoseshi hata lepe la usingizi kwamba Mwafrika hana haya kuchukia mwenzake?

Mauaji ya wageni wa Kiafrika yanayoendelea Afrika Kusini hayakupi tafakuri kuhusu thamani anayojipa Mwafrika kabla ya kuwanyoshea wengine kidole cha lawama?

Upendo ni bora kuliko chuki; nao wivu ni kidonda, yeyote anayeshiriki hukonda.

[email protected]