Maoni

MUTUA: Mzozo katika UDA utakufanya udhani Ruto anastaafu kesho!

June 1st, 2024 2 min read

NA DOUGLAS MUTUA

YAANI hii Kenya imegawanyika hivi kwamba, mtu hawezi kuzungumza ukweli pasi na kushukiwa kuwa anaunga mkono mrengo fulani wa kisiasa.

Mfano bora ni kisa ambapo Katibu Mkuu wa chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA) amewakemea mawaziri wawili walio na ukuruba na Rais William Ruto kwa kumshambulia Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Sasa Bw Malala amebatizwa kibaraka wa Bw Gachagua, sikwambii tayari baadhi ya watu wanaamini anaegemea upande huo na wala si ule wa Rais.

Wapo pia wanaoshangaa iwapo Bw Malala amemsaliti mshirika wake wa kisiasa, Waziri wa Mambo ya Nje, Bw Musalia Mudavadi, anayeaminika alimwezesha kupata cheo cha ukatibu anachotumia kuwakomesha watu anaoamini ni maadui wa Bw Gachagua.

Bw Malala amewakanganya wengi kwa kumkemea Gavana wa Nyeri, Bw Mutahi Kahiga, ambaye ni mshirika mkuu wa Bw Gachagua.

Ajabu akidi ni kwamba, sijamsikia yeyote akimtetea Bw Malala kwa hoja kwamba, ni katibu wa chama tu anayetekeleza majukumu yake ya kuwarudi wanachama watundu inavyostahili.

Ugomvi unaoendelea sasa hivi ni changamano mno kwa sababu unaaminika kuwa siasa za urithi, yaani watu kujiandalia kuchukua hatamu za uongozi wa nchi hii wakati Dkt Ruto ataondoka mamlakani.

Shughuli hizi zimezidi mno ndani ya muungano wa Kenya Kwanza ambao unatawala wa nchi kwa kuwa washirika katika muungano wenyewe wanaamini Dkt Ruto ataongoza nchi mpaka 2032.

Utadhani Kenya haina Upinzani Rasmi, wala wanasiasa walio nje ya muungano huo, ambao pia wana ndoto za kumwondoa Dkt Ruto mamlakani katika Uchaguzi Mkuu wa 2027.

Jambo ambalo wengi wanaogopa kusema ni kuwa, siasa hizo za urithi katika Kenya Kwanza zinaongozwa na Bw Gachagua kwa upande mmoja, na Bw Mudavadi, kimya-kimya, kwa upande wa pili.

Na kwa sababu Kenya ni nchi ya kikabila, watu wanamshangaa Bw Malala akionekana kumuunga mkono Bw Gachagua, mtu wa Mlima Kenya.

Hata hivyo, hawamshangai Bw Kuria kwa kuwa alijulikana hata kabla ya serikali ya sasa kuundwa alikuwa adui wa kisiasa wa Bw Gachagua.

Nadhani anayetazama sinema inayoendelea na kucheka kwa raha zake ni Bw Mudavadi kwa kuwa ana watetezi wengi, hapondwi na yeyote kwenye kambi yake, yaani anasubiri tu kuona itakuwaje mwishowe.

Bw Gachagua hawezi kuketi kitako na kutazama yanayoendelea kwa sababu amekalia kiti ambacho kimeyawasha makalio ya wanasiasa tangu Kenya iwe huru.