Makala

MUTUA: Ni unafiki viongozi kujifanya hawajawahi kutusi awali

September 12th, 2020 2 min read

Na DOUGLAS MUTUA

UNAFIKI wa viongozi wakuu unatishia kuigawa Kenya mafungu kadhaa hasimu ambayo yatakuwa vigumu kudhibitika kati ya sasa na uchaguzi mkuu ujao.

Rais Uhuru Kenyatta, Naibu Rais Dkt William Ruto na mkuu wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) Bw Raila Odinga wameonyesha unafiki mkuu.

Watatu hao, ambao kwa hakika ni mafundi wa kutukana hata matusi ya nguoni, sasa wamo mbioni kuharamisha matusi kana kwamba wamepigwa na radi iliyompiga mtesi wa Wakristo, Saulo, akabadili mienendo yake na kuwa Paulo.

Rais Kenyatta, ambaye pamoja na familia yake wametokea kutukanwa na kudhihakiwa na viongozi wasiokubaliana naye kisiasa, amewahi kuingia lawamani kwa kumtusi Raila, viongozi wengine na hata wananchi wa kawaida.

Raila naye amewahi kujipata pabaya kwa kumtusi mwendazake Daniel Moi, Rais Mstaafu Mwai Kibaki, Dkt Ruto na hata Uhuru mwenyewe kabla ya kuridhiana naye.

Dkt Ruto, mtu na ulimi wa moto, ametukana kuanzia Moi, Kibaki na Raila, akajizuia tu kumtapikia nyongo Bw Kenyatta kwa kuwa ndiye mkuu wake sasa na siasa za urithi zingalipo.

Kila mtu aliye na akili razini, hata za kubabaisha tu, anajua viongozi hao wanatumia mbinu zozote zitakazowawezesha ama kusalia mamlakani au kuyapata mamlaka ifikapo 2022.

Utadhani sasa wamekuwa walokole, tayari katika safari ya kwenda mbinguni, na hivyo vijembe vya kisiasa ambavyo wamepigana miaka hii yote ni dhambi kuu asiyopaswa kufanya Mkenya.

Lawama unazosikia dhidi ya Mbunge wa Emurua-Dikirr, Bw Johana Ng’eno, na mwenzake wa Kapseret, Bw Oscar Sudi, zimekuweko tangu enzi ya marehemu Jomo Kenyatta.

Hii ina maana kwamba matusi yamekuwa nasi tangu wakati huo. Kila anapotukanwa mtu mashuhuri nchini, watetezi wake hulenga kunufaika kwa njia moja au nyingine.

Raila anamtetea Uhuru dhidi ya matusi ya Bw Ng’eno na Bw Sudi si kwa sababu anampenda sana bali anatarajia kuwa ushirikiano wao wa kisiasa utampa (Raila) urais.

Na ni lazima Raila asisitize kwamba Bw Ng’eno na Bw Sudi wametumwa na Dkt Ruto kumtukana Uhuru na familia yake kwa kuwa Dkt Ruto ndiye mshindani wake mkuu.

Dkt Ruto naye, japo labda hajali Uhuru akitukanwa, amewakosoa marafiki zake hao kwa kuwa anataka kuonekana kama anayemheshimu mkubwa wake.

Heshima za nini ilhali Uhuru mwenyewe ameonyesha wazi hamheshimu wala kumpenda Dkt Ruto? Naibu Rais anajua akimvunjia heshima mkuu wake hadharani hatapata kura nyingi za eneo la Mlima Kenya hapo 2022.

Ni sawa kutumia mbinu kali kumwangusha mwenzako kwenye mchezo mchafu wa siasa, lakini Raila anakosea anaposisitiza kwamba matusi yataanzisha vita nchini.

Huo ni uchochezi usio na msingi na unaonuiwa kumsawiri Dkt Ruto kama mtu hatari asiyefaa kuiongoza nchi.

Ananuia kuwakumbusha Wakenya kuhusu vita vya kisiasa vilivyotokea eneo la Rift Valley mnamo 2007 bila kuwaambia yeye na Dkt Ruto walikuwa washirika wakati huo.

Baba yake mwenyewe, Jaramogi Oginga Odinga, JM (Josiah Mwangi) Kariuki, Pio Gama Pinto, Koigi Wamwere na wengine walipomkosoa na hata kumtusi Jomo hawakunuia kuleta vita nchini. Wala washirika wake wa sasa kama vile Mbunge wa Embakasi Mashariki, Bw Babu Owino, Bi Millie Odhiambo wa Mbita, Junet Mohamed wa Suna Mashariki na Gavana wa Mombasa, Hassan Joho.

Mbunge wa zamani wa Limuru, Bw George Nyanja, aliposema Moi asipobadilika atabadilishwa na mabadiliko hakunuia kuzua vita nchini.

Kenya ni taifa la kipekee kote barani Afrika; tunajulikana kwa ukakamavu wa kuwakabili viongozi wetu na hata kuwaambia mambo yasiyoandikika.

Watanzania husema hatuna adabu eti. Lakini huo ndio uhuru wetu na hatupaswi kumruhusu yeyote atupokonye au tumwombe msamaha kwa kuutumia.

Labda ndiyo sababu Kenya haijawahi kutawaliwa na majeshi kwa kuwa wanajua watakuwa na kibarua kigumu kutudhibiti. Hatunyamazishwi na hatutishiwi kamwe.

Yeyote asiyepita kiwango cha kukerwa na matusi anapaswa kujiuliza iwapo anataka kuongoza Kenya.

Nalo taifa lililo na sheria zinazowakataza watu kutukanana linapaswa kukomaa na kutunga sheria mpya.

[email protected]