Makala

MUTUA: Polisi wa Kenya wanastahili medali kwa kudhulumu raia

May 30th, 2020 2 min read

Na DOUGLAS MUTUA

JUZI nimedhihakiwa na mtani fulani kwamba tangu nihamie Marekani nimeanza kufikiria kama wazungu.

Kisa na maana nililinganisha mauaji yanayozuilika ambayo hutokea nchini Kenya na Marekani, nikasema maisha ya raia wa Kenya yamo hatarini zaidi.

‘Nilitupa jiwe polisi’ nilipokariri kwamba rafiki yangu Ken Walibora aliishi Marekani kwa muda mrefu na hakuuawa, aliporejea Kenya akafariki kifo kichungu!

Haya yalitokea wakati wa mjadala ulioibuliwa na visa vitatu vya ubaguzi wa rangi dhidi ya watu weusi nchini Marekani ambapo wawili waliuawa.

Mbali na habari za janga la corona, nyingine zinazogonga vichwa vya habari Marekani ni kisa cha George Floyd kubanwa shingoni kwa goti na afisa wa polisi hadi kufa!

Kipo pia kisa cha Ahmaud Arberry, 26, aliyeuawa kwa kupigwa risasi na wazungu wakati akifanya mazoezi ya kukimbia mnamo Februari ila kikafichwa na polisi mpaka hivi majuzi.

Kisa cha tatu kinamhusu Christian Cooper, muungwana aliyemwona dada wa kizungu akimtembeza mbwa bila ugwe kama inavyotakiwa, akamshauri amfunge.

Kisha? Msichana wa watu alimtishia Cooper kwamba angemuitia polisi, eti awaambie: “Mimi na mbwa wangu tunatishiwa maisha na mwanamume mweusi.”

Simu ilipoingia tu, msichana huyo kwa jina Amy alianza kulia huku akimsogelea Cooper na kumsihi aliyekuwa upande wa pili wa simu awatume polisi upesi!

Polisi walipofanya uchunguzi walibaini kwamba Cooper hakufanya kosa lolote, Bi Amy ndiye aliyetia chumvi kadhia yote hiyo kutokana na ubaguzi wa rangi.

Visa hivyo vitatu vimewaudhi wengi kote duniani. Na kwa sababu vinaripotiwa wakati mmoja, utadhani Marekani ni jehanamu, kwamba tunaoishi huku tunateketea.

Nimewaona Waafrika wengi wakiapa eti hata wakipawa fursa za kuishi huku hawawezi kukubali kwa sababu watahatarisha maisha yao. Inaeleweka.

Aliyetushauri tuzoee kuyatoa maboriti yaliyo ndani ya macho yetu kabla ya kuvitoa vibanzi kwenye macho ya wenzetu aligonga ndipo. Nyani haoni kundule hasa!

Mwanzo tuelewane: Ni kweli kuwa ubaguzi wa rangi upo mwingi tu Marekani, na kwamba wahanga mara nyingi ni watu weusi. Kuna uhusiano wa mbwa na chui kati ya watu weusi na weupe nchini humu.

Baadhi ya watu weusi, hasa vizazi vya watumwa waliojenga Marekani bila kulipwa chochote, huwa na kisasi na wazungu.

Nao baadhi ya wazungu huwachukia na kuwaogopa watu weusi kiasi cha kuwasingizia uhalifu kwa jumla, au hata kuwaambia warejee walikotoka.

Hata hivyo, tunapolinganisha polisi wa Kenya na Marekani wanavyowatendea watu, tunakuta kwamba Kenya kumeoza!

Kila Mkenya anaweza kutoa mfano wa kisa ambapo ama alibughudhiwa au akashuhudia mtu akihangaishwa na polisi bila sababu yoyote.

Ikiwa unaishi kwenye nchi ambapo wakili na wateja wake wanauawa na polisi kwa kushughulikia kesi ya uvunjaji wa haki za binadamu, una boriti ndani ya jicho. Litoe!

Ikiwa unaishi ndani ya nchi ambapo mashahidi wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) wanauawa na hivyo basi kesi dhidi ya watu mashuhuri kufeli, una kazi.

Unapoishi kwenye nchi ambapo vikosi maalum vya polisi – mathalan Kwekwe, Flying Squad, na Pangani Six – vinaundwa kwa minajili ya kuwaua wahalifu badala ya kuwakamata na kuwashtaki mahakamani, kwenu kumeoza.

Marekani hakuna kikosi hata kimoja cha kuwaangamiza washukiwa kabla ya kesi zao kusikilizwa kikamilifu na kuamuliwa.

Mara moja-moja utakutana na polisi waovu Marekani, lakini aghalabu mwisho wa kila kisa unategemea mtakavyojibizana. Kenya unapigwa hata kabla ya kutamka neno.

Polisi wengi Marekani, hata ukiwatukana matusi ya nguoni, ilmradi unatii maagizo yao, hawajali. Jaribu kufanya hivyo Kenya!

 

[email protected]