Habari Mseto

Mutua, Raila wakutana na kujadili masuala ya 'kupeleka taifa mbele'

July 18th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

HATUA ya Gavana wa Machakos Alfred Mutua kumtembelea kiongozi wa ODM Raila Odinga imepewa fasiri ya maandalizi ya kinyang’anyiro cha urais mwaka 2022.

Hii ni baada ya Dkt Mutua kutoboa kwamba kati ya masuala ambayo walijadili afisini mwa Bw Odinga katika jumba la Capitol Hill, Nairobi, Jumatano ni siasa.

“Nilisaka ushauri wake kuhusu mipango yangu ya kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2022. Nilimpa ratiba ya mipango yangu,” Dkt Mutua akafichua.

Duru zilisema kuwa Bw Odinga alimhakikishia Gavana Mutua kwamba atakuwa tayari kushirikiana naye kama “mshauri na mshirika” kwa ajili ya kumsaidia Mutua kunadi sera zake kote nchini.

Viongozi hao wawili waliafikiana kuwa mfumo bora wa utawala ni ule usiotenga maeneo mengine ya nchi.

Chini ya mfumo huo Dkt Mutua na Bw Odinga walipendekeza kuwa uongozi ujao uwe na Rais aliyechaguliwa pamoja na Waziri Mkuu na Manaibu wake wawili.

“Huu mfumo wa sasa ambapo mshindi katika uchaguzi mkuu ndiye hudhibiti vyeo vyote serikali ndio chanzo cha matatizo ambayo yamekuwa yakilizonga taifa hili kila baada ya uchaguzi,” akasema Bw Odinga.

Chanzo cha matatizo

Wawili hao walilaani siasa za zinazojengeka kwa ukabila wakisema ndio chanzo cha matatizo ambayo yamelikumba taifa hili kwa kipindi kirefu hata baada ya ujio wa utawala wa vyama vingi kuanzia miaka ya tisini (1990s).

“Inasikitisha kuwa siasa za nchi hii imekuwa ikiendeshwa kwa misingi ya kikabila wala sio misingi ya sera na maongozi. Mustabali wa taifa hili utabainishwa kwa misingi ya namna tunavyoendesha siasa zetu,” Dkt Mutua akasema kwenye ujumbe aliouchapisha katika ukurasa wa akaunti yake ya mtandao wa Twitter.

Kiongozi huyo wa chama cha Maendeleo Chap Chap alimsifu Bw Odinga akimtaja kama kiongozi shupavu na mwenye maono mazuri kwa taifa hili.

“Hii ndio maana nimedumisha uhusiano wa karibu na Bw Odinga tangu tulipohudumu pamoja katika serikali ya muungano akiwa Waziri Mkuu nami nikishikilia wadhifa wa Msemaji wa Serikali,” Dkt Mutua akaeleza.

Gavana huyo alisema kuwa Bw Odinga alikubali kutembelea Kaunti ya Machakos katika tarehe ambayo haijaamuliwa.