Makala

MUTUA: Serikali iitikie kilio cha Wakenya walio Lebanon

August 15th, 2020 2 min read

Na DOUGLAS MUTUA

NIMEANDIKA na kurudia hapa kwamba maisha ya Mkenya aliye ugenini hayana thamani kwa Serikali ya Rais Uhuru Kenyatta.

Ni kana kwamba mtu akivuka mpaka tu ndio basi uhusiano wake na nchi yake unakatika mara moja na akijipata katika hali tatanishi ajihangaikie kivyake mpaka awe salama.

Ikiwa huamini, jiulize kwa nini mwanahabari Yassin Juma angali kizuizini Ethiopia hata baada ya mahakama kuagiza aachiliwe, nao Wakenya wengine wanatukanwa na kuambiwa hakuna msaada wao, eti wakitaka waandamane usiku kucha nchini Lebanon!

Ni aibu iliyoje kuona Wakenya wakihangaikia kwenye barabara za jiji la Beirut huku wakiililia Serikali yao iwarejeshe nyumbani?

Si hayo tu! Serikali ya Kenya imewapa sharti kuu: kabla ya kuruhusiwa kuabiri ndege ili kurejea nyumbani, lazima uwe na stakabadhi safi za kusafiria.

Na wamekumbushwa kwamba hilo ni sharti linalozingatiwa kimataifa kabla ya mtu aliye katika hali yao hiyo kutia guu kwenye ndege yoyote.

Hii ina maana kwamba ikiwa huna stakabadhi hizo, basi jikalie huko uliko barabarani tu.

Wakenya hao wamejipata katika hali hiyo baada ya mlipuko uliotokea hivi majuzi jijini Beirut ukaharibu eneo kubwa na na kuwaacha wengi bila kazi wala makao.

Je, Serikali ya Kenya haiaibiki kwamba raia hao wamejenga vibanda vya kuishi kwa muda kando ya barabara wakitumia bendera za Kenya?

Kweli Serikali ya Kenya inadhani watu hao ni raia wa nchi nyingine ambao wametumia bendera hizo kwa kusidi la kuiaibisha nchi hii?

Mwanzo hilo dai la Serikali ya Kenya kwamba sharti la kimataifa linalomhitaji mtu kuwa na stakabadhi za kusafiria kabla ya kuabiri ndege lina kasoro.

MADAI YA UONGO

Naam, kasoro kwa sababu ni dai tu, tena lina nusu ya ukweli, si ukweli kamili.

Ni kweli kwamba mtu anayenuia kusafiri kwa ndege ya kawaida hawezi kuruhisiwa kuiabiri bila paspoti au akiwa na paspoti iliyokwisha muda wake wa kutumika.

Lakini mtu anayesafiri kwa ndege maalum – mathalan ya kijeshi au iliyokodishwa kwa shughuli maalum kama uokoaji, hapewi sharti hilo.

Kitu ambacho Serikali ya Kenya haitaki kufanya ni kutuma ndege maalum Beirut kwa shughuli ya kuokoa watu wetu. Haitaki kugharamika sana, inataka kulipia mtu mmoja-mmoja nauli na ndiyo sababu inawaagiza waathiriwa watimize sharti hilo la usafiri wa umma.

Kenya ingekuwa inawathamini raia wake, ndege ya kijeshi ingetua Beirut siku moja baada ya kilio cha Wakenya walio huko kusikika ili iwarejeshe nyumbani mara moja!

Lakini tukio hili la Lebanon lisikushangaze. Tuliona kujikokota kwa aina hiyo pale ilipobainika kwamba Wakenya wengi walikuwa wamekwama mjini Wuhan, Uchina, mwanzoni mwa janga la corona. Unajua masaibu yaliyowasibu ndugu zetu huko.

Linganisha hali hizo na aliyokuwa Bw Raila Odinga, mshirika wa kisiasa wa Rais Uhuru Kenyatta, hivi majuzi ukitilia maanani kwamba Serikali ilikodi ndege maalum ili kuwasafirisha Gavana wa Mombasa, Bw Ali Hassan Joho, na Mbunge wa Suna Mashariki, Bw Junet Mohammed, kwenda kumwona hospitalini.

Kenya, kutokana na ufisadi na maovu mengine yaliyo serikalini, imeshindwa kubuni nafasi za kazi na mazingira bora ya mtu binafsi kujiendeleza.

Wakenya wanapotafuta mbinu na kwenda kuzumbua riziki nje ya nchi wanafaa kuhakikishiwa angalau ulinzi na msaada wanapouhitaji.

[email protected]