Makala

MUTUA: Tafiti za afya hasa kuhusu Ukimwi zastahili kuifaa jamii

October 26th, 2019 2 min read

Na DOUGLAS MUTUA

UTAFITI umefanywa juzi ukaonyesha kwamba kampeni ya kupambana na Ukimwi kwa kuwapasha tohara wanaume wengi imekuwa na matokeo hatari.

Hapa nazungumzia watu wazima ambao ama waliichangamkia fursa ya kutahiriwa au wakakubali shingo upande tu kwa kusadikishwa kuna manufaa ya kiafya.

Wanaopambana na Ukimwi wametuambia kwa muda mrefu kwamba mwanamume aliyekatwa govi anapungukiwa na hatari za kuambikizwa ugonjwa huo.

Inakisiwa kwamba huo ndiyo msukumo ambao umewashawishi wanaume wengi duniani kuingia utu uzima uzeeni.

Nchini Uganda, asilimia kubwa ya wanaume waliokubali kukutana na kisu cha ngariba waliamini basi, tahadhari haina haja tena, wakazama kwenye ngono bila kinga!

Mipira ya kondomu ambayo imekuwa maarufu nchini humo kwa miongo zaidi ya miwili ilitupiwa dirishani, majembe yakaingia mashambani kulima tuputupu eti. Maskini!

Kwa mujibu wa baraza la mapambano dhidi ya Ukimwi nchini Uganda (UAC), idadi ya wanaume wa kati ya miaka 40 – 50 walioacha kutumia kinga wakati wa ngono baada ya kupashwa tohara ni asilimia 24.

Sasa wataalamu wa afya wana hofu kubwa kwamba huenda takwimu za baadaye zikaonyesha ongezeko la maambukizi mapya, ambayo yalikuwa yameshuka pakubwa.

Uganda ilikabiliwa na hatari kubwa ya kuangamizwa na ugonjwa huo miaka ya tisini, lakini serikali ya Yoweri Museveni kwa msaada wa mashirika ya kimataifa ilidhibiti hali.

Miaka hiyo ungewasikia Wakenya wakitahadharishana dhidi ya kujamiiana na Waganda au yeyote aliyezuru taifa hilo jirani kwani waliogopa kuambukizwa.

Kilio cha Waganda kilisikika na mashirika kama lile la Umoja wa Mataifa la afya duniani (WHO), lile la Marekani la misaada ya kimataifa la USAID na kadhalika, hali ikatengenea.

Unyanyapaa huo dhidi ya Waganda ulififia polepole na raia wa Afrika Mashariki wakaanza kutangamana bila wasiwasi, lakini huenda mambo yakabadilika na historia ikairudia.

Kwa muda mrefu nimeamini kwamba wataalamu wa kimataifa wanaokuja Afrika kutoa ushauri na misaada mbalimbali wanapaswa kuelewa watu walivyo kwanza.

Shughuli za kusaidia na kuelimisha watu zinaweza kuwa madhubuti sana iwapo wenyeji watafundishwa mambo na kueleweshwa kikamilifu kuhudu madhara na manufaa yote.

Vinginevyo, kisu kilichonuiwa kukatia nyanya na vitunguu kitatumiwa kupasua kuni huku shoka likikatia nyanya na vitunguu.

Kwa mfano, kuna fundisho moja kuhusu Ukimwi ambalo limeendelea kwa muda mrefu na huenda lina madhara makubwa kwa watu, haswa wanaume.

Upotoshi

Wataalamu wa kupambana na Ukimwi wakidai kwa muda mrefu kwamba mwanamume hayuko katika hatari ya kuambukizwa Ukimwi iwapo hatalala na mwanamke kwa mara 13 mtawalia bila kinga.

Ingawa wanawake wakitahadharishwa zaidi kwa kuambiwa kuwa, kwa sababu za kimaumbile, wao wako katika hatari kubwa ya kuambikizwa hata bila kuingiliwa kikamilifu, kuna shida.

Shida ni kwamba huenda wanaume wakora, ama ukipenda beberu wajanja, wamejasiria kujaribisha hadi mara ya 12 na kung’oa kucha ikisalia mara moja pekee.

Swali kuu: Wataalamu wana hakika gani kwamba mara hizo 12 ni salama? Waliwapima watu wangapi kabla ya kuzuka na tangazo hilo? Kina dada nao wanusurikeje?

Tangazo hilo la salama ya mwanamume, hadi kufikia jaribio la 12, pamoja na hilo jingine la tohara, ni hatari mno hususan katika jamii iliyo na elimu duni na taarifa chache.

Tafiti za kina zinapaswa kufanywa kwanza kisha walengwa waelimishwe kikamilifu kabla ya kutangaziwa mambo yanayowaondolea tahadhari na kuwaingiza mitegoni.

Nimeandika kwa muda mrefu sana kwamba siwaamini watu wengi wanaojiita wataalamu wa mapambano dhidi ya maradhi. Yao imekuwa tasnia, kitega uchimi haswa!

Kisa na maana ni kwamba wasingetaka kupoteza kazi, nazo kampuni zinazotengeza dawa na vifaa vingine kama mipira ya kondomu zinataka kubakia kwenye biashara milele.

Jiulize kwa nini maradhi kama Malaria ambayo yalitafutiwa tiba zamani hayajaangamizwa kikamilifu; unayosikia mara kwa mara ni matoleo mapya ya dawa za kuyatibu.

 

[email protected]