Makala

MUTUA: Tanzania ni jirani jeuri, tuvumilie kuishi naye

August 1st, 2020 2 min read

Na DOUGLAS MUTUA

NCHI inapojipata na jirani mbaya ilhali yenyewe haiwezi kuhama au kumhamisha, inapaswa kufanya nini?

Nimeandika hapa kwa takriban miaka mitano sasa, tangu Dkt John Pombe Magufuli achaguliwe rais Tanzania, kwamba taifa hilo si rafiki bali adui.

Japo halijatangaza uadui wa wazi, kuna mifano kadhaa ya mambo ambayo ukijumuisha moja na moja, utapata hesabu kamili: Tanzania si rafiki wa Kenya.

Juzi tu, ujumbe wa waombolezaji kutoka Kenya uliokuwa njiani kuelekea Tanzania kuhudhuria ibada ya wafu ulirudishwa nchini katika hali isiyoeleweka vyema.

Nimesema hali isiyoeleweka vyema kwa sababu waelekezi wa safari za ndege nchini Tanzania walisema hali mbaya ya hewa haingeruhusu ndege hiyo ya Kenya kutua.

Ujumbe huo ulikusudia kumwakilisha Rais Uhuru Kenyatta katika ibada ya kumuaga aliyekuwa rais wa tatu wa Tanzania, Bw Benjamin Mkapa.

Uliongozwa na kiongozi wa wengi kwenye Bunge la Seneti, Bw Samuel Poghisio, na ulisafiri kwa mojawapo ya ndege maalumu zinatotumiwa na rais wa Kenya na watu mashuhuri. Ndege hiyo, ambayo tayari ilikuwa imevuka mpaka na kuingia Tanzania, ilinyimwa ruhusa ya kutua hivyo ikabidi irejee ilikotoka.

Katika juhudi za labda kuficha uzito wa tukio hilo, Bw Poghisio alidai ujumbe wake uliagizwa ama urejea Kenya au usubiri hewani kwa muda.

Na kwa sababu kwenye Bunge la Seneti kulipangiwa kuwa na majadiliano muhimu kuhusu ugavi wa pesa za ugatuzi, alidai Bw Poghisio, alilazimika kurejea Kenya.

Wataalamu wa masuala ya kiutawala na kidiplomasia watakwambia hakuna shughuli muhimu nchini kokote kuliko kumwakilisha kiongozi wa nchi kwenye hafla ya kimataifa.

Kikawaida, mjumbe aliyetumwa na kiongozi wa nchi hufanya kila juhudi kuhakikisha ametekeleza wajibu wake. Kisa na maana ni kwamba anaiwakilisha nchi.

Kwa kifupi tu, tunaweza kusema Tanzania iliizuia Kenya kuhudhuria ibada ya wafu ya rais wake wa tatu, Mzee Mkapa.

Hebu niseme moja kwa moja kwamba, binafsi nalitilia shaka dai hilo la hali ya hewa kuwa mbaya. Safari hiyo haikuwa ya kushtukiza; hali ya hewa inatabiriwa hata wiki mbili kabla.

Vile vile, kuna njia kadhaa za ndege kupitia ili kutua kwenye uwanja wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Katika ulimwengu wa kidiplomasia, nchi ikitaka kuidharau nyingine, huwatuma wawakilishi wa ngazi ya chini kwenye hafla za nchi inayolengwa.

Nchi hiyo nayo ikishuku tu kwamba hizo ni dharau, hukazana kuidhalilisha iliyozuka na dharau, hivyo hali ikawa ya vita baridi.

Nashuku kwamba kwa upande wa Kenya, hili ni suala la tahadhari tu kuhusiana na janga la Corona, hasa ikizingatiwa kwamba Tanzania na jeuri yake imesema hakuna Corona.

Kumbuka Kenya ilipofunga mpaka wake na Tanzania, taifa hilo la Magufuli liliteta vikali na kuzuia yeyote au chochote kutoka Kenya mpaka Rais Kenyatta akalazimika kuingilia kati.

Haikosi Kenya ililazimika kumtuma Bw Poghisio na ujumbe wa watu wawili pekee badala ya Rais Uhuru Kenyatta kuhudhuria ibada hiyo na kuhatarisha maisha yake.

Hapa unatambua kuwa kuhusiana na jirani mkorofi, ni lazima uwe mwangalifu sana. Katika kisa hicho cha juzi, Kenya ilikabiliwa na hatari mbili za kumkasirisha jirani huyo: siasa za corona na maadili ya kidiplomasia.

Hatua ya pekee ambayo ingekubalika machoni pa Tanzania na Rais Magufuli ni Rais Kenyatta mwenyewe ahudhurie ibada hiyo au amtume Naibu wake, Dkt William Ruto.

Tukubaliane kwamba shughuli muhimu za nchi haziwezi kuwa kuifurahisha nchi nyingine, ndiposa naiunga mkono hatua ya Rais Kenyatta kutofika.

Hata hatua ya kutuma ujumbe Tanzania haikufaa kitu; hakuna maisha ya Mkenya ambayo yanapaswa kuhatarishwa ili tuifurahishe nchi nyingine. Tuna jirani mbaya, hebu tubuni mikakati ya kumdhibiti.

[email protected]