Makala

MUTUA: Tuliyojifunza Ghana si lazima vifo uchaguzini

December 12th, 2020 2 min read

Na DOUGLAS MUTUA

MATAIFA mengi Afrika yanapaswa kujifunza mengi kutokana na uchaguzi wa urais uliofanyika Ghana hivi majuzi.

Kwa mtazamo wa Mwafrika aliyezoea ghasia kila wakati wa uchaguzi, huo uliofanyika ndani ya taifa hilo la Afrika Magharibi ulipooza mno.

Ikizingatiwa kuwa Rais Nana-Akufo Addo alikuwa anatafuta kuchaguliwa kutumika kipindi cha pili na cha mwisho.

Kikawaida, marais wengi wa Afrika wanapotetea vyeo vyao lazima afe mtu! Utadhani dunia nzima inapaswa kusimama ili mtetezi huyo afaulu, maisha yaendelee akifanikiwa.

Hebu angalia jirani yetu Uganda! Museveni, ambaye anawania urais kwa mara ya sita, ndiye mwanzilishi mkuu wa ghasia na ukiukaji wa haki za binadamu.

Mpinzani wake katika uchaguzi utakaofanyika Januari 14 ni Robert Kyagulanyi ama kwa jina la msimbo Bobi Wine, kijana aliyekuwa mtoto wa shule ya msingi mzee wa watu alipotwaa mamlaka kwa mtutu wa bunduki 1986.Ukiona mambo ambayo Museveni anamfanyia Bobi, ikiwemo kukamatwa na polisi na baadhi ya wafuasi wake kuuawa, utadhani hakuna Uganda bila mzee huyo.

Kila wakati polisi wanaziba barabara kumzuia Bobi asifike maeneo anakopangiwa kuhutubia wafuasi wake.

Hatimaye anapita vichochoroni na kuhutubia watu vijijini, mbali na alikokusudia.

Hata wasimamizi wa hoteli wametishiwa na Museveni hivi kwamba hawamruhusu Bobi kulala humo anapofanya kampeni mbali na nyumbani kwake.

Juzi, picha zake zilisambaa mtandaoni zikimwonyesha kavuta usingizi mnono ndani ya gari usiku kucha. Mwaniaji mzima wa urais! Na akishinda? Wala asikwambie mtu; Bobi anafanyiwa yote hayo kwa sababu Museveni ameshaamua kuwa ushindi ni wake hata ikiwa Bobi atapata kura nyingi kumzidi.

Sasa unaweza kuelewa kwa nini kuna Waganda wengi wanaishi nchi za watu kama wakimbizi wa kisiasa.

Hilo la wakimbizi wa kisiasa nalo ni jingine nyeti tu! Angalia hali ilivyo kwa jirani yetu Tanzania; wanasiasa wanatishiwa maisha.

Bw Godbless Lema, ambaye alikuwa mbunge wa upinzani hadi alipoibiwa kura na kuhangaishwa mnamo Oktoba 2020 sasa ni mkimbizi wa kisiasa nchini Canada.

Bw Lema na familia yake walikimbilia Kenya walipotishiwa maisha.

Bw Tundu Lissu, aliyewania urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema); alikwisha kimbilia Ubelgiji akiogopa kuuawa.

Unasalitika kujiuliza iwapo huu ni mwaka wa 2020! Wakenya tulipitia hayo miaka ya 80.

Hata hivyo ni sisi tuliomwapisha usiku Rais Mwai Kibaki aliyeshindwa katika Uchaguzi Mkuu wa 2007. Maafa yaliyoandama yameingia kwenye kumbukumbu za historia tayari.

Lakini kwa sababu tuna ugumu wa kijifunza, sasa tumo mbioni kuhalalisha haramu ya mtawala kunata mamlakani kiujanja baada ya muda wake kustaafu.

Nimesema tujifunze na Ghana kwa kuwa, japo wana historia ya mapinduzi ya kijeshi, waliipisha demokrasia na kuiruhusu inawiri.

Nchini humo, ukifika muda wa rais kustaafu, mwenyewe huwa amechoka tu na anataka kuondoka.

Waafrika, hasa kichaa wa Afrika Mashariki, wanapaswa kufahamu kuwa siasa si uadui na kutenda kila jambo kwa maslahi ya nchi.

[email protected]