MUTUA: Tunashangilia madikteta wakipinduliwa ila ipo hofu

MUTUA: Tunashangilia madikteta wakipinduliwa ila ipo hofu

Na DOUGLAS MUTUA

KIMOJA kati ya vichekesho ambavyo vimetokea kuvutia sana kwenye mitandao ya kijamii ni picha za watu wakiigiza jeshi la Guinea likimkamata Rais Alpha Conde.

Rais Conde alipinduliwa wiki jana na kukamatwa na kikosi maalum ambacho kikimlinda, mtandaoni kikaweka picha zake akiwa mahabusu hoi, si amiri jeshi mkuu.

Badala ya watu kumwonea imani kiongozi huyo kwa kuwa wanajeshi hao walitisha kwa silaha nzito-nzito, walifurahia hali yake na kuiona kioja kikuu.

Nchini Guinea kwenyewe hali ilikuwa shangwe, vifijo na nderemo huku wanawake wakiahidi kuwatuza wanajeshi hao kwa huduma isiyoandikwa ikaandikika hapa.

Mbona wawatuze wanajeshi kwa kumpindua rais aliyechaguliwa?

Mbona watu wamwagike mitaani kushangilia haramu? Si kuihalalisha huko?

Imekuwa desturi kwa raia kushangilia na kuwatuza wanajeshi wanaojasiria kupindua serikali dhalimu.

Wapo wanaowapa wanajeshi vyakula, vinywaji na kadhalika.

Ushangilizi ambao hufanyika, hasa Afrika, kila serikali inapopinduliwa ni kitendawili kigumu kuteguliwa na mataifa ya magharibi.

Hayaelewi fikra na mienendo yetu.

Kwa makadirio yao, utawala wa kijeshi unatabirika kuwa dhalimu kuliko wa dikteta mwingine anayepinduliwa kwani nguvu ni kigezo kikuu katika kuwadhibiti raia.

Hata hivyo, Mwafrika amenyanyasika kwa muda mrefu hivi kwamba yeyote, hata ibilisi, anayejitoa mhanga kumwondolea mtesi wake hukaribishwa kwa mikono miwili.

Ushangilizi huo hauwi wa kumwidhinisha nduli mpya aendelee kumkalia mguu wa kausha Mwafrika bali ile raha tu ya kumuona mtesi akilipia dhambi zake.

Iwapo anayemwadhibu mtesi atageuka mtesi mpya huwa si hoja wakati huo, muhimu kwa mshangilizi ni kwamba manyanyaso aliyokumbana nayo yatasitishwa.

Kwa aliyeteswa akakinai, pumziko la hata saa chache tu humpa matumaini ya kuwa na mustakabali bora kuliko dhiki aliyozoea.

Fikra za aina hii ziliwasababisha Waganda kumshangilia Iddi Amin alipompindua mtesi wao, Dkt Milton Obote.

Hawakujua kwamba Amin angewaua kinyama halafu.

Raia wa Ghana pia walishangilia pale Dkt Kwame Nkurumah alipinduliwa na wanajeshi baada ya kugeuka dikteta.

Huyo naye akidhani hadhi ya kuwa mwanzilishi wa taifa ilimwidhinisha kuisimamia nchi kama shamba lake la mpunga; alikaa miaka kadha bila kuteua makamu wake.

Mapinduzi mengi yaliyotokea Nigeria pia yalishangiliwa na raia wakitamani kumwona mtesi wao akiona cha mtema kuni.

Walikuwa radhi kupambana na hali yao halafu.

Hayo ni matukio ya miongo kadha iliyopita, muda mfupi tu baada ya mataifa mengi ya Afrika kuwa huru, hivyo raia hawakuwa wameupevuka akili umuhimu wa utawala bora.

Mwafrika wa leo amejanjaruka akajua kitu muhimu kinachoitwa katiba, kisichoruhusu maonevu na manyanyaso yoyote yale na wanafahamu fika anayewadhulumu anakikiuka.

Waafrika wamefahamu ni haramu kwa kiongozi wa nchi kubadili katiba ili kunata mamlakani, hivyo hata akifanikiwa kuibadili kinyume na mapenzi yao anavunja sheria.

Mfano bora ni kisa cha juzi nchini Guinea ambapo Rais Conde, mzee mzima wa umri wa miaka 83, alibadili katiba mwaka 2020 baada ya kutawala kwa mihula miwili ili apate wa tatu.

Alifanikiwa kufanya hivyo na hatimaye akashinda uchaguzi ambao upinzani ulisema ulikosa uhuru na uwazi. Walioandamana kumpinga ama waliuawa au wakafungwa jela.

Je, bado unashangaa kwamba kupinduliwa kwa dikteta huyo kulizua sherehe ghafla? Maskini raia wa Guinea walimpisha mwenye nguvu wasivunjwe mbavu bure ila wakabaki na vijiba vya roho wakijua hakuna mtesi atesaye kufululiza. Yamemfika ghafla, wanaona raha si haba.

Wanatarajia wanajeshi hao wawafanyie haki kwa kuwarejeshea utawala, hatua inayoweza kufanikishwa haraka na Muungano wa Kiuchumi wa Mataifa ya Afrika Magharibi (ECOWAS).

Wanajeshi hao, ikiwa waliingia mamlakani kutokana na uzalendo na wala si uchu wa mamlaka, wanapaswa kusalimu amri ya ECOWAS badala ya kuwekewa vikwazo.

mutua_muema@yahoo.com

You can share this post!

Japan yasitisha mpango wa kuwa mwenyeji wa fainali za Kombe...

Chebukati aonya dhidi ya kampeni hizi za mapema