Makala

MUTUA: Utashinda kesi ukikana mashtaka ya kusingiziwa

December 19th, 2020 2 min read

Na DOUGLAS MUTUA

KISA cha binti kumsingizia babake ubakaji na hivyo kusababisha afungwe jela maisha ni kionjo tu cha maovu ambayo hutokea kwenye mahakama zetu.

Bw Julius Wambua Musyoki aliachiwa huru juzi na Jaji wa Mahakama Kuu, Bw George Odunga, baada ya Ushahidi kuonyesha kwamba binti yake alishawishiwa ili kumsingizia makosa.

Binti ya mtu alifanikiwa kumtia babake jela maisha yapata miaka minane iliyopita kutokana na ushawishi wa mamake kwa kuwa wanandoa hao walikuwa na mzozo.

Bi Dorcas Mwende aliiambia mahakama kwamba wazazi wake walikuwa na mzozo, hivyo mamake mzazi akamshawishi kudai kwamba babake, Bw Musyoki, alimbaka.

Kusudi la madai hayo mabaya, ambayo yalitolewa na msichana huyo akiwa na umri wa miaka 16 na yakaaminiwa na mahakama, lilikuwa mama atwae mali ya mumewe.

Na mama mtu alifanikiwa kwa kiasi kikubwa hadi pale nafsi ilipoanza kumhukumu binti yake, akaamua kusema ukweli, ambao umemweka huru babake juzi.

Kisa cha Bw Musyoki ni kimoja tu kati ya vingi ambavyo hutokea nchini Kenya, mtu akafungwa kwa makosa ya kusingiziwa, akasahaulika na mara nyingine kufia jela.

Mara nyingi huwa polisi wamevuruga uchunguzi au ukosefu wa uchunguzi wa kisayansi kama vile vipimo vya chembechembe za DNA na kadhalika.

Linalonizuga akili kabisa ni hatua ya hakimu au jaji anayeshughulikia kesi kama hii na kumfunga mtu jela bila kuzingatia vitu vya kimsingi kama uchunguzi wa DNA.

Wakati mwingi kishawishi huwa hongo, lakini pia mapuuza ya haki za binadamu huchangia maamuzi mabaya kama hayo.

Binadamu ana hulka ya kumhukumu mtu akilini hivi kwamba akiambiwa fulani katenda hili au lile, hata kabla ya kuchunguza yaliyojiri, mawazo yake humshawishi kuamini mshukiwa ana hatia.

Hizo ni fikra za kawaida za binadamu, lakini afisa wa mahakama kama jaji au hakimu anapaswa kuwa mkomavu kutokana na utaalamu wa kazi na ufahamu wake wa jamii yetu iliyozama kwenye maovu.

Kishawishi kingine cha maafisa wa mahakama kutoa uamuzi mbaya ni ufisadi. Si siri kwamba mahakama za Kenya zimejaa mafisadi wasio na haya hata kidogo.

Wanapopokezwa kiinua mgongo, mshukiwa huhukumiwa na kupatwa na hatia hata kabla hajafikishwa mahakamani.

Ikizingatiwa kwamba vitabu vitakatifu vya imani kuu nchini Kenya vinaonya dhidi ya ushahidi wa uongo na maamuzi maonevu ya kesi, unashawishika kujiuliza kwa nini anayetoa na kupokea hongo hajirudi?

Hongo

Lakini ndicho chanzo cha maovu yote, hivyo aliye na hela hupata anachotaka hata kama ni kunyanyasa watu mradi ana fursa ya kufanya hivyo.

Inaonekana tutashuhudia maamuzi mabaya ya mahakama kwa muda mrefu kwa kuwa hata mara chache ambapo idara ya mahakama imepigwa msasa, haijaleta manufaa yoyote.

Sinuii kuilaumu idara ya mahakama pekee kwa kuvuruga utendaji haki nchini. Mbali na kuwezeshwa na mafisadi, wananchi wa kawaida wasio na uwezo wa kuhonga pia huiwezesha.

Hata afadhali Bw Musyoki aliyejaribu mara kadhaa kupata haki kwa kukataa mashtaka na pia kukata rufaa alipohukumiwa visivyo; Wakenya wengi hukubali makosa ili kesi iishe.

Kuna woga ambao Mkenya ameishi nao miaka mingi tu, yaani kuhofia kwamba akikanusha mashtaka atatupwa rumande na kutesekea humo kwa muda mrefu.

Ukitaka kuamini hili, tembea siku moja kwenye mahakama yoyote inayoshughulikia kesi za waliovunja sheria za usalama barabarani.

Hata kabla ya mashtaka yenyewe kumaliza kusomwa, washtakiwa wengi huyakubali mara moja na kutangaziwa faini wanazopaswa kulipa.

Wapo wengine ambao hushtuka ghaya ya kushtuka wakikubali mashtaka bila kutafakari kuhusu ubaya wa hatua hiyo au wa mashtaka yenyewe na kutupwa jela kwa muda mrefu.

Ukikabiliwa na mashtaka ya kusingiziwa, yakatae kabisa uendelee na kesi hadi mwisho. Usikiri makosa usiyotenda, utatozwa faini haramu. Tumia pesa hizo kujiwekea dhamana.

Wengi wanaokusingizia ama huchoshwa na kesi, huhukumiwa na nafsi zao wenyewe na kukuacha, au hushindwa kuwahonga maafisa wa mahakama kwa muda mrefu.

[email protected]