Makala

MUTUA: Wafisadi hawana aibu tena, watafuna bila kupepesa jicho

August 29th, 2020 2 min read

Na DOUGLAS MUTUA

IWAPO umekuwa ukitoa Somalia kama mfano wa taifa lililoporomoka, sasa itabidi utafute taifa jingine.

Huko kwa kuporomoka kumeanza kutokwa na sidhani kutarejewa.

Huku Wakenya wakiendelea kucheka kwa hasira kutokana na kuporwa kwa pesa zilizonuiwa kukabiliana na janga la Corona, Wasomali wanafanya mambo.

Taifa hilo jirani hivi majuzi liliwafunga jela pamoja na kuwatoza faini maafisa wanne wa serikali waliohusika na kashfa inayofanana na hiyo ya Kenya – wizi wa pesa za Corona.

Kenya nako? Hamna kitu! Ahadi tu kutoka kwa Rais Uhuru Kenyatta aliyewatolea makataa ya siku 21 wapelelezi wakamilishe uchunguzi.

Iwapo kuna watu walioamini vitisho vya Bw Kenyatta vingeathiri chochote, basi ni wachache mno; anajulikana kwa kuapa kukabiliana na mafisadi huku akiuma mdomo wa chini lakini wapi!

Amewahi kunukuliwa wakati mmoja akiuliza Wakenya wanataka afanye nini kuhusu ufisadi nchini.

Hatujasahau kwamba kashfa ya kwanza kutokea kwenye Wizara ya Afya wakati wa utawala wake, ya jumla ya Sh5 biliojni, ilisahaulika kimiujiza dada yake alipoibuka kuwa mshukiwa mkuu.

Wasomali hawakuhitaji rais wao kuingilia kati ili mafisadi watiwe ndani; idara ya mahakama ilifanya kazi yake, kufumba na kufumbua, waovu wakajipata wakijiandaa kutengana na familia zao kwa muda mrefu.

Mkurugenzi wa Utawala wa Wizara ya Afya Somalia, Bw Mohamoud Bulle Mohamoud, 52, alifungwa jela miaka 18 na akaagizwa alipe faini sawa na shilingi za Kenya laki mbili na nusu. Naye Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya ya Somalia, Bw Abdullahi Hashi Ali, 61, alifungwa jela miaka tisa na pia akaagizwa alipe faini ya shilingi laki mbili unusu za Kenya. Fisadi wa tatu, Bw Mahdi Abshir Mohamed, 30, aliyekuwa msimamizi wa mradi huo wa kupambana na Corona, alifungwa jela miaka 12 na kutozwa faini sawa na wenzake.

Mwizi wa mali ya umma wanne, Bw Bashir Abdi Nur, 34, aliyekuwa mkuu wa idara inayoshughulikia malaria na virusi vya Ukimwi, alifungwa jela miaka mitatu na kutozwa faini sawa na shilingi za Kenya laki moja na elfu ishirini. Hayo ni majina ya watu ambao kila mwananchi wa Somalia anaweza kuthibitisha wapo kwa sababu walifanya kazi na serikali ila wakacheza visivyo. Wa Kenya hatuwajui!

Cha kutamausha zaidi, mafisadi wa Kenya wamewapata watetezi wapya – Raila Odinga na chama chake cha Orange Democratic Movement.

Tangu ajiunge na Serikali ya Jubilee kwa mlango wa nyuma, Raila sasa hajui makosa yoyote ya utawala aliotumia miaka zaidi ya sita akikashifu kwa maovu mbalimbali.

Anacholenga sasa hivi ni kutimiza ndoto yake ya kuwania urais kwa mara ya tano ifikapo 2022, shughuli ambayo nadhani kwake ni muhimu kuliko usalama wa mali ya Mkenya.

Asichojua ni kwamba, hao wanaoiba huku akiwaangalia tu ili wakati huo ukifika wamkabidhi urais hawana mipango kama hiyo, watamsaliti mchana jua la utosi!

Lakini Wakenya watakumbuka daima kwamba wagonjwa wa janga la Corona waliibiwa na Serikali, Raila ama alikaa kimya au alikuwa miongoni mwa wezi.

Amelaaniwa anayemtegemea mwanadamu, Biblia takatifu inasema. Mkenya amelaaniwa kwa kumtegemea Raila amtatulie matatizo serikalini kana kwamba mwenyewe hana maslahi binafsi ya kujali.

Cha mno ni kwamba, Raila amezeeka, hana tena zile nguvu za ujana za kumvaa kila anayeleta masihara. Kazi sasa ni kujipongeza kimyakimya kwa kazi ngumu ya miaka mingi.

[email protected]