MUTUA: Wakenya walio ng’ambo wana haki ya kupiga kura

MUTUA: Wakenya walio ng’ambo wana haki ya kupiga kura

Na DOUGLAS MUTUA

NILICHEKA kidogo kisha nikakereka kweli-kweli hivi majuzi kutokana na matamshi ya mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Bw Wafula Chebukati.

Akiongea na makundi ya kidini, Bw Chebukati aliahidi kwamba angewapa haki za kupiga kura, katika uchaguzi ujao, Wakenya wanaoishi nje ya nchi.

Wanaoishi kwenye mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na Afrika Kusini walishiriki chaguzi kuu za 2013 na 2017.

Kwa walio kwingineko Afrika, Marekani, Uropa, Asia, Mashariki ya Kati na kadhalika, hiyo imesalia ndoto isiyoagulika – hadaa baada ya hadaa, na hadaa zaidi.

Serikali ikidai haina uwezo wa kifedha kuendesha shughuli hiyo kokote waliko Wakenya milioni 3.5, lakini ikipokea kwa pupa ushuru wanaolipa kwa mamilioni.

Sikwambii mfuko mnono unaotengewa tume ya uchaguzi huishia kuwa kitoweo cha watu wabadhirifu wanaoitafuna nchi kana kwamba kiyama chaja kesho.

Sasa Bw Chebukati anadhani amefanya kitu cha maana sana kutangaza huenda wanaoishi Marekani, Canada, Sudan Kusini, Uingereza, Qatar na Muungano wa Mataifa ya Kiarabu (UAE) wakamchagua rais mwaka 2022.

Nilicheka kwa kuwa nilidhani hiyo ni danganya-toto ya kawaida ambayo tumeisikia tangu mwaka wa 2010 tulipoipitisha Katiba ya sasa.

Huwa raha ukihadaiwa ukajua.

Yaliyoniudhi hadi ya kuniudhi ni matamshi ya ‘kuwapa haki ya kupiga kura Wakenya wanaoishi ughaibuni’.

Yangetolewa na kabwela wa watu ningemmpuuza tu, hazidishi hapunguzi! Lakini Bw Chebukati ndiye mkuu wa uchaguzi hasa, tena wakili anayeielewa Katiba sawasawa.

Anajikweza sana mtu wa kiwango chake anapodai atawapa haki Wakenya walionyanyasika miaka yote hii ilhali anajua ni haki yao ya kikatiba.

Hata heri angetanguliza kwa kuomba msamaha kwani amekiuka Katiba miaka mingi tu kwa kutoweka mikakati ya kuwawezesha Wakenya kupata haki hiyo.

Hii si mara ya kwanza kwa ahadi kama hiyo kutolewa, lakini kila uchaguzi unapokaribia vinavyoandamana ni visingizio.

Hata baada ya makundi kadha ya Wakenya kuishtaki serikali mahakamani wakidai haki hiyo, wasimamizi wa uchaguzi wametokea kushupaa shingo na kupuuza kilio hicho.

Kupanga mikakati ya Wakenya kupiga kura kokote waliko hakuigharimu serikali kama miradi ambayo imeishia kufyonzwa na kupe wanono wanatao kwenye nundu ya umma.

Tatizo ni ukosefu wa utashi wa kisiasa; wanasiasa hawaoni tija katika kuwawezesha Wakenya walio ughaibuni kushiriki upigaji kura.

Hakika, wanasiasa wanawaogopa watu hao kwa kuwa wanadhani wamepambazukiwa na dunia kwa kuishi nchi za watu ambako mambo hufanywa tofauti na kwa uwazi.

Kwa makadirio ya wanasiasa, watu milioni 3.5 walioonja ubora wa maisha nje ya nchi ni hatari ikilinganishwa na ‘kondoo’ wa mtaani waliozoea kupelekwa machinjioni kimyakimya kila baada ya miaka mitano.

Wanasiasa huhofia kuwa watu hao, kutokana na mtagusano wao na watu wa asili nyingine, wanaweza kuukiuka ukabila wakamchagua mwaniaji aliye na sera bora.

Na kwa kuwa wanasiasa wetu ni wakora wasiojiamini, hawana hakika sera zao zinaweza kuwashawishi Wakenya hao, hivyo ni heri waliwe njama, watulize boli huko waliko.

Ukiwaona waambie wasihofu kwa kuwa huku nje tumetengana kishenzi tu, tumeshindwa kuuacha ukabila, hata makundi ya WhatsApp tunaunda kwa misingi ya makabila yetu!

Wanasiasa pia huogopa uwezo wa kifedha wa wanaoishi ughaibuni kwani, kinyume na wanavyofanya nchini, wanasiasa hawawezi kwenda kuwagawia vihela vyao huko nje.

Kwa jumla, Wakenya tumelimatia sana kudai haki zetu za kimsingi kama hii ya kupiga kura.

Tumezembea kuwawajibisha wanasiasa wetu, wakatugawa mafungu, sasa wanacheza nasi kama mwanasesere.

Wataanza kutuheshimu tutakapoacha uzembe na upofu wa kupanga tuliojitwika, tudai haki zote za kimsingi hata zisizotufaa moja kwa moja.

mutua_muema@yahoo.com

You can share this post!

Watu 7 wauawa katika shambulio la kigaidi Mogadishu

KAMAU: Ni aibu kuwatelekeza mashujaa waliopigania uhuru