Habari MsetoSiasa

Mutula Kilonzo ajitetea kumwakilisha Sonko

December 22nd, 2019 1 min read

Na PIUS MAUNDU

SENETA Mutula Kilonzo Junior wa Makueni amejitetea vikali dhidi ya shutuma za kumwakilisha Gavana Mike Sonko kwenye kesi ya ufisadi inayomkabili.

Seneta huyo amejipata lawamani pamoja na mwenzake Kipchumba Murkomen (Elgeyo Marakwet) na mbunge Daniel Maanzo (Makueni) baada yao kuungana na mawakili waliomwakilisha Bw Sonko kwenye kesi hiyo.

Mbali na tuhuma za ufisadi, gavana huyo anakabiliwa na shtaka la kuwashambulia polisi wakati alipokuwa akikamatwa majuma mawili yaliyopita.

Miongoni mwa walioonekana kukasirishwa na hatua hiyo ni Rais Uhuru Kenyatta.

Kwenye hotuba yake wakati wa sherehe za Sikukuu ya Jamhuri, Rais Kenyatta alisema kuwa haifai watumishi wa umma kujihusisha katika masuala ya kibiashara wakiwa bado katika ofisi.

“Mwanasheria Mkuu anapaswa kuharakisha Sheria ya Kudhibiti Matumizi Mabaya ya Mamlaka na kuuwasilisha kwa taasisi husika kama Bunge la Kitaifa ili kujadiliwa” akasema Rais. Agizo hilo lilijiri siku moja baada ya Bw Sonko kuachiliwa kwa dhamana.

Hata hivyo, Bw Kilonzo anasema kuwa hatabadilisha msimamo wake hata kidogo.

“Hatukumwakilisha Bw Sonko kwa kupuuza sheria. Polisi walimhangaisha walipokuwa wakimkamata. Nilitaka aachiliwe ili aweze kujitetea akiwa huru,” akasema Bw Kilonzo.

Seneta huyo alisema alimwakilisha Bw Sonko ili kuhakikisha kuwa haki na usalama wake umezingatiwa.

Alimtaja gavana huyo kama rafiki wa kifamilia kwa muda mrefu na mtu ambaye huwa anajitolea sana kuwasaidia wale ambao hawajiwezi katika jamii. Alisema alihisi kuna haja ya kuhakikisha usalama wake kutoka kwa vikosi vya usalama.