Muturi adai uhasama umeathiri Bunge

Muturi adai uhasama umeathiri Bunge

Na WANDERI KAMAU

SPIKA wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi, Alhamisi alikiri kuwa tofauti za kisiasa kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais William Ruto zimeathiri utendakazi wa Bunge.

Bw Muturi alisema kuwa tofauti za wawili hao zimewaathiri sana baadhi ya wabunge ambao walikuwa wakijitolea sana katika kuitetea serikali hapo awali.

Kwenye mahojiano na kituo kimoja cha redio Alhamisi, Bw Muturi alieleza amejaribu sana awezavyo kuwapatanisha wawili hao ijapokuwa hajafaulu hadi sasa.

“Baada ya kugundua tatizo lililokuwepo Bungeni, nilijaribu njia zangu mwenyewe kuwapatanisha wawili hao mnamo Janauari ijapokuwa sikufaulu. Nilikusanya viongozi kadhaa wa kidini ijapokuwa juhudi zetu ziligonga mwamba. Wote wawili walishikilia misimamo mikali,” akasema Bw Muturi.

Spika alionya hali hiyo imeathiri uendeshaji wa baadhi ya ajenda za serikali, kwani imemlazimu kutumia nguvu na kunyenyekea ili kuwarai baadhi ya wabunge kuunga mkono hoja hizo.

“Si hali ya kuridhisha wakati unalazimika kumrai mbunge aliyekuwa akijitolea kuitetea serikali kuunga mkono ajenda ya serikali yenyewe. Imeathiri sana mshikamano wa kisiasa ambao ulikuwepo awali,” akasema, akiongeza wengi wao wamepoteza motisha waliokuwa nao mara tu baada ya uchaguzi wa 2017.

Kauli yake inajiri huku baadhi ya viongozi wa kidini wakiripotiwa kuanza upya juhudi za kuwapatanisha wawili hao, nchi inapoelekea kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Viongozi ambao wanaoongoza juhudi hizo wanaonya huenda ikawa hatari kwa nchi kuelekea kwenye uchaguzi huo chini ya migawanyiko iliyopo kwa sasa.

Juhudi hizo zinaripotiwa kuongozwa Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki katika Dayosisi ya Nyeri, Anthony Muheria.

“Hakuna anayefaidika kutokana na hali ilivyo nchini. Ni vizuri zoezi muhimu kama uchaguzi lifanyike katika mazingira yenye utulivu na uthabiti wa kisiasa,” akasema Askofu Muheria.

Rais Kenyatta amekuwa akimlaumu Dkt Ruto kwa kumkaidi kwa kuendeleza kampeni za 2022, huku Dkt Ruto akilmaulu Rais kwa “kumnyang’anya” majukumu yake na kumkabidhi Waziri wa Usalama wa Ndani, Fred Matiang’i.

You can share this post!

Museveni akemea mapinduzi Guinea

Mjukuu wa Moi adai hana uwezo kulea watoto