Habari

Muturi amtaka Yatani aunde hazina maalum ya kuweka fedha kutoka kwa mishahara iliyokatwa

March 28th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

SPIKA wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi amemtaka Waziri wa Fedha Ukur Yatani abuni hazina maalum ambapo pesa zitakazopunguzwa kutoka kwa mishahara ya maafisa wakuu wa serikali zitahifadhiwa.

Mnamo Alhamisi, Muturi na mwenzake wa Seneti Ken Lusaka walitangaza kuwa wamehiari kupunguza mishahara yao kwa kiasi cha asilimia 30 ili kupiga jeki vita dhidi ya virusi vya corona.

Walitoa tangazo hili siku moja baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutangaza kuwa yeye na naibu wake William Ruto watapunguza mishahara yao kwa asilimia 80 kila mmoja kama hatua ya kuunga mkono mpango wa kudhibiti kuenea kwa virusi hivyo.

Vilevile, alisema mishahara ya mawaziri, wasaidizi wao na makatibu wa wizara itapunguzwa kwa kati ya asilimia 30 na 20 kwa ajili ya mpango huo.

Sasa Bw Muturi anasema Waziri Yatani ndiye mwenye mamlaka kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Umma (PFM act) ya 2012 kubuni hazina maalum ya kuelekeza fedha zitakazopunguzwa kutoka kwa mishahara ya maafisa hao.

“Nchi hii haina historia nzuri kuhusiana na maamuzi kama haya. Lakini ninatarajia kwamba Hazina ya Kitaifa itabuni hazina maalum ambapo pesa hizo zitakazopatikana chini ya mpango huu zitahifadhiwa kwa matumizi yaliyokusudiwa,” akasema Bw Muturi kwenya taarifa iliyowekwa kwenye tovuti ya bunge.

Mwenyekiti wa Baraza la Magavana Nchini (CoG) Wycliffe Oparanya pia ametangaza kuwa magavana wote nchini wamehiari kupunguza mishahara yao kwa kiasi cha asilimia 30 ili kupiga jeki mpango wa kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona.