Muturi awekewa presha aungane na Ruto, si Raila

Muturi awekewa presha aungane na Ruto, si Raila

Na ALEX NJERU

WANASIASA wa Mlima Kenya sasa wanasema kuwa Spika wa Bunge la Kitaifa, Bw Justin Muturi anaandaliwa na Rais Uhuru Kenyatta kuwa mwaniaji mwenza wa kinara wa ODM Raila Odinga.

Wanasiasa wa mrengo wa Tangatanga eneo la Mlima Kenya Mashariki wanasema kuwa wanasita kumpigia debe Bw Muturi kutokana na hofu kwamba huenda wakamsaidia Bw Odinga kujipa umaarufu katika eneo hilo.

Akizungumza wakati wa hafla ya kuchangisha fedha kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ya Shule ya Upili ya Nthaara, eneobunge la Taharaka – uliohudhuriwa na Bw Muturi –mbunge wa Tharaka, Bw Gitonga alimtaka Spika wa Bunge la Kitaifa, kuunga mkono Dkt Ruto.

Alidai kuwa eneo la Mlima Kenya linaunga mkono Dkt Ruto hivyo basi Bw Muturi anastahili kuwa mwaniaji mwenza wa Naibu wa Rais.

“Tunakutaka kujiunga na vuguvugu la Hasla ili mfanye mazungumzo na Dkt Ruto uwe mwaniaji wake mwenza,” akasema Bw Murugara.

Katika mahojiano na Taifa Leo, Mwakilishi Mwanamke wa Tharaka Nithi, Beatrice Nkatha, alisema anataka Bw Muturi kushirikiana na Naibu Rais ili kuunda serikali ijayo.

“Muturi ni kiongozi bora na yeye ndiye yuko katika nafasi nzuri ya kuwa mwaniaji mwenza wa Dkt Ruto. Lakini inaonekana Muturi ni kibaraka wa Rais Kenyatta ili kumfanya mwaniaji mwenza wa Bw Odinga,” akasema Bi Nkatha.

Bw Muturi amesisitiza kuwa ataendelea na juhudi zake za kuwa rais 2022 na ataendelea kuzungumza na viongozi wenye maono sawa na yake ili kubuni muungano.

Alisema hatafanya mazungumzo na viongozi ambao anafahamu vyema kwamba wanaongozwa na maslahi ya kibinafsi.

“Ninakubali kwamba viongozi wanaowania viti mbalimbali hawana budi kuketi chini na kuzungumza lakini mimi nitazungumza tu na wanasiasa walio na maono sawa na yangu,” akasema.

Alisema viongozi wanafaa kutoa kipaumbele kwa maslahi ya wananchi wala si yao wenyewe.

“Kila kiongozi pia anafaa kuwa katika mstari wa mbele katika kuhakikisha uchaguzi unakuwa wa amani na wawe tayari kukubali matokeo,” akasema.

Mbunge wa Mbeere Kaskazini, Bw Muriuki Njagagua na mwenzake wa Kirinyaga ya Kati, Bw Munene Wambugu, na Mkurugenzi wa Makavazi ya Kitaifa, Dkt Mzalendo Kibunjia ambao pia walihudhuria hafla hiyo walimtaja Bw Muturi kama kiongozi mwenye maono, mchapakazi na mnyenyekevu huku wakihimiza watu wa eneo la Mlima Kenya kumuunga.

Bw Njagagua aliwataka viongozi wote wa eneo la Mlima Kenya kuunga mkono Bw Muturi huku akijiandaa kuwania urais kumrithi Rais Kenyatta mwaka ujao.

“Inasikitisha kuona baadhi ya viongozi wa Mlima Kenya wakipinga Bw Muturi ilhali wanajua kwamba yeye ndiye tegemeo letu baada ya Rais Kenyatta kustaafu 2022,” akasema Bw Njagagua.

Bw Wambugu alimtaka Bw Muturi kuunganisha watu wa Mlima Kenya ili anyakue kura zote mwaka ujao.

Bw Muturi ameapa kuwa ataunganisha eneo la Mlima Kenya ili wampigie kura 2022 huku akisisitiza kuwa watu wa eneo hilo wamekuwa pamoja hata kabla ya Kenya kupata uhuru na hataruhusu wakazi kugawanywa na wanasiasa.

You can share this post!

Wazozana kuhusu ufanikishaji miradi

Viongozi wa kidini wasuta wanasiasa kupepeta corona