Siasa

Muturi aziba mwanya ambao wabunge hutumia kutafuna maelfu

October 12th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

SPIKA Justin Muturi ametoa amri kwamba ni wabunge saba pekee wataruhusiwa kusafiri maeneo mbalimbali nchini kushughulikia masuala yaliyoko mbele ya Kamati za Bunge la Kitaifa.

Kanuni hiyo inalenga kudhibiti gharama ya usafiri wa wabunge humu nchini na ng’ambo, ili kuokoa mabilioni ya fedha ambayo wabunge hufuja katika safari kama hizo kila mwaka.

Bw Muturi ameziagiza kamati za bunge kuunda kamati ndogo zitakazosimamia safari za wanachama wao humu na kimataifa.

“Vile vile, wenyeviti wa kamati watalazimika kuwa katika mikutano ambayo wanachama wao watafanya nje ya majengo ya bunge. Idadi fulani ya wafanyakazi wa bunge pia watahudhuria mikutano,” kanuni hiyo mpya inasema.

Spika Muturi alimwagiza Karani wa Bunge la Kitaifa Michael Sialai kuwasilisha mwongozo huo kwa kamati zote za bunge na ahakikishe kuwa kanunuzi zote zilizomo zinatekelezwa.

Katika mwaka wa kifedha wa 2019/2020 asasi ya bunge ilitumia Sh5.3 bilioni kugharamia safari za humu nchini, kulingana na ripoti ya Msimamizi wa Bajeti (CoB).

Fedha hizo zilijumuisha Sh1.5 bilioni zilizotumiwa na Tume ya Huduma za Bunge (PSC) na Sh3.4 bilioni zilzotumiwa na Bunge la Kitaifa.

Kwa kuwa safari nje ya nchi zimezimwa kutokana na janga la Covid-19, wabunge wameelekeza macho yao katika safari za humu nchini kama njia ya kupata fedha zaidi.

Wabunge hulipwa marupurupu (per diem) ya Sh5,000 kila siku wanapofanya ziara za humu nchini nje ya Nairobi. Gharama ya malazi hulipiwa na PSC.

Katika bajeti ya mwaka huu wa kifedha wa 2020/2021 bajeti ya safari ilipunguzwa hadi Sh2.8 bilioni kama njia ya kuachilia fedha zaidi za kuelekezwa kufadhili mikakati ya kupambana na makali ya Covid-19.