Habari Mseto

Mutyambai aonya wanaothubutu kuviteketeza vituo vya polisi

July 14th, 2020 2 min read

Na SAMMY WAWERU

INSPEKTA Mkuu wa Polisi (IG) Hillary Mutyambai ameonya wanaothubutu kuviteketeza vituo vya polisi.

Bw Mutyambai amesema hatua hiyo inakiuka sheria, na kwamba “wanaofanya hivyo wasitarajie kusazwa”.

Visa kadhaa vya umma kuteketeza vituo vya polisi, kwa kile kimetajwa kama maafisa kudhulumu raia katika utekelezaji wa kafyu ya kitaifa na pia sheria na mikakati kuzuia msambao wa Covid-19, vimeshuhudiwa.

Tukio la hivi punde ni la mauaji ya mtu mmoja katika kituo cha polisi cha Rioma, Kisii, ambapo umma wenye ghadhabu uliishia kuchoma kituo hicho.

Taswira sawa na hiyo ilishuhudiwa eneo la Lessos, Kaunti ya Nandi, ambapo mkazi mmoja alidaiwa kuuawa na maafisa wa polisi.

Ilisemekana mwathiriwa alikuwa mhudumu wa bodaboda, na alipigwa risasi kwa sababu ya kubeba wateja wawili, kinyume na kanuni ya Wizara ya Afya wahudumu wa bodaboda kutakiwa kusafirisha mtu mmoja kwa awamu ili kuzuia kuenea kwa virusi vya corona.

Aidha, umma ulioghadhabishwa na mauaji hayo ulichoma nyumba ya afisa msimamizi wa kituo hicho na jaribio la kuteketeza hifadhi ya bunduki na silaha lilitibuka.

Ni kufuatia matukio hayo IG Mutyambai ameonya umma dhidi ya kuchukua sheria mikononi.

“Ninaonya umma unaochukua sheria mikononi na kuchoma kituo cha polisi, bila shaka makali ya sheria yatachukua mkondo,” Bw Mutyambai akatahadharisha Jumatatu usiku kwenye mahojiano na runinga ya Citizen.

Katika visa vya Lessos-Nandi na Rioma-Kisii, jaribio la kuchoma vituo hivyo baadhi ya wahusika walijeruhiwa vibaya na kadhaa kuuawa kufuatia makabiliano makali kati yao na polisi.

“Walikiuka sheria kuteketeza kituo cha polisi, walitarajia nini itokee kufuatia kitendo cha aina hiyo?” IG alihoji.

Bw Mutyambai alisema wajibu wa maafisa wa polisi ni kulinda mali, kando na kusaidia kutekeleza sheria. Alisema kisheria kuna utaratibu uliowekwa kueleza lalama za maafisa wa polisi wanaohujumu na kudhulumu raia.

“Ninasihi raia ishirikiane na idara ya polisi. Kuna njia halali kueleza malalamishi,” akahimiza.

Maafisa husika katika kituo cha polisi cha Lessos walisimamishwa kazi, huku Mamlaka Huru ya Usimamizi na Uangalizi wa Polisi (IPOA) ikianzisha uchunguzi.

Bw Mutyambai alisema IPOA inaendelea kuchunguza visa vya maafisa wanaotajwa kutumia nguvu kupita kiasi na kudhulumu raia wakati wa utekelezaji kafyu.

“Kuna kesi nyingi za maafisa walioadhibiwa kinidhamu, hata ingawa siwezi kufichua majina na nambari zao za usajili katika idara ya polisi,” akasema. Alihakikishia taifa kwamba chini ya uongozi wake kama Inspekta Mkuu, anafanya kila awezalo kuhahakikisha kikosi cha polisi NPS kinaimarika na pia kuimarisha uhusiano kati ya polisi na raia.

Visa vya vituo vya polisi nchini Kenya kuanza kuchomwa vimejiri mwezi mmoja baada ya raia wenye asili ya Kiafrika Marekani kuteketeza kituo cha polisi cha Minneapolis, kufuatia mauaji ya kinyama ya mmoja wao, George Floyd chini ya maafisa wa polisi.